WATU wengi wanapoanza kufanya biashara wanakuwa hawafanyi utafiti wa kutosha, matokeo yake biashara wanazozianzisha zinakufa. Hivyo basi, biashara unayoifanya ni vema ukazingatia vitu mbalimbali kabla ya kuifungua, ikiwamo eneo la biashara, samani pamoja na muonekano wake kwa wateja wako.
Baadhi ya watu wanaoanza biashara zao wanakuwa na makosa yanayojirudia mara kwa mara kwa kupangisha ofisi za gharama kubwa, kununua samani za bei kubwa na vifaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa vipeperushi vya thamani kwa lengo la kuujulisha umma kuhusu biashara hiyo, bila kuangalia bajeti aliyojiwekea kwa biashara husika. Lakini ni vema kujua mbinu na kanuni za kufanya biashara ili uweze kusonga mbele badala ya kurudi nyuma, ama kuifunga baada ya muda mfupi.
Mara nyingi wateja wanapenda kufanya biashara na watu wenye utaalamu wa biashara husika. Maana yake ni kwamba, mteja huyo anamuona mfanyabiashara huyo kuwa yuko makini na anaijali biashara yake.
Lakini kama tabia ya biashara yako ipo kinyume cha hali hii, yaani mfanyabiashara mwenyewe si mtaalamu wa biashara yake, wateja humkimbia. Mfanyabiashara unaweza ukaiweka biashara yako katika mtazamo ule unavyotaka iwe, mfano jinsi unavyovaa, sehemu iliyopo na vifaa unavyovitumia, ni tafsiri tosha ya biashara yako iko vipi.
Pia unaweza kutumia fani yako ikakubalika kwa wateja uliowakusudia. Kwa mfano, kama unaanzisha mgahawa mdogo wa kuwahudumia wateja wa kawaida kama wafanyakazi wa ujenzi, hutakiwi katika biashara yako uwafanye wajisikie hawako huru.
Ingawa katika mgahawa wako una uwezo wa kuwawekea uma na visu, usifanye hivyo kama wako huru zaidi kutumia vijiko ama mikono yao. Mfano mwingine, kuna saluni moja ya kifahari ilishindwa kusonga mbele kwa kuwa wamiliki hawakuzingatia mahitaji ya wateja walio nao.
Katika saluni hiyo waliiweka katika daraja la juu na kujenga tafsiri kuwa wanaoingia humo ni wale tu wenye pesa zao, badala ya kulenga wateja wa eneo hilo husika, ambao walikuwa ni watu wa kawaida. Hivyo hawakuwapata wateja wale waliowakusudia, pia wale wa kawaida ambao hawakuwalenga, kwa kuwa waliwadharau kuanzia mwanzo.
Hapa jambo lililokuwa linatakiwa ni kuwaweka katika mizani moja wateja wote wa daraja la kawaida na daraja la juu. Kufanikiwa kwa biashara kunatokana na mwonekano wake. Kama mfanyabiashara unatakiwa kujenga mwonekano mzuri wa biashara unaoutaka, kwa kuonesha kuwa hilo ni eneo la fani yako.
Jambo jingine linalosababisha biashara zisiendelee ni pale mhusika anaposhindwa kupata soko la uhakika. Unaweza kuzalisha bidhaa za viwango vya juu pamoja na kutafuta masoko kwa wingi, lakini ukawa hauna soko la uhakika.
Utafiti unaonesha kuwa, wafanyabiashara wengi wanaanza biashara kwa kufanya utafiti wa juu juu bila kujiridhisha uhitaji wa biashara anayotaka kuianzisha kama atapata wateja au la.
Matokeo yake anatumia mtaji mkubwa, muda na nguvu wakati huo biashara hiyo inakuwa ndogo. Nini kifanyike? Kabla ya kuanza biashara inatakiwa ufanyike utafiti wa kutosha wa kujua kama soko litakuwapo, ukubwa wa soko hilo na uimara wake.
Huhitaji kufanya utafiti wenye gharama kubwa. Unatakiwa kuzungumza na wateja wako kwa kuwauliza ni kwa kiasi gani wananunua bidhaa hizo na mara ngapi. Zungumza na wasambazaji na washindani wako. Jua biashara nyingine zinakwenda vipi na jinsi gani wanaboresha masoko yao.
Kushindwa kwa bidhaa inawezekana inatokana na kushindwa kwa biashara. Sababu ya kushindwa kwa bidhaa inawezekana ni kutokana na maelezo ya mfanyabiashara husika, bidhaa yenyewe au soko.
Hali hiyo ukikutana nayo labda uwe na bidhaa nyingine inayokuingizia kipato, ni vema kubadili biashara kuliko kuacha kabisa kufanya biashara. Viashiria vifuatavyo huchangia kushindwa kwa biashara.
Viashiria hivyo ni kuanzisha biashara katika muda mbaya ama kwenye kipindi kibaya cha hali ya hewa ya biashara husika, kulenga kundi ambalo sio sahihi, kutumia mikakati dhaifu, bei mbaya, kushindwa kuitangaza, kuiinua ama kuweka utayari wa bidhaa husika kwa wateja ili waweze kujua thamani na faida za bidhaa husika, pamoja na matarajio yasiyofikia malengo.
Kabla ya kuzindua bidhaa, ni vema kufanya utafiti ili kujua watu wanataka nini. Asilimia kubwa ya wafanyabiashara hawajui soko lao linahitaji nini, hivyo wanazalisha kile wanachodhani soko linahitaji, kuliko kujua soko linataka nini.
Lakini wakati mwingine, ni vigumu kujua soko liko vipi hata baada ya kufanya utafiti. Mfano mzuri ni pale unapochapisha, wachapishaji hufanya utafiti, lakini bado vitabu vinakataliwa na wasomaji bila sababu za msingi.
Kuzuia kupata hasara zaidi, unashauriwa kuchapisha kiasi kidogo cha vitabu na kujua mwitikio wa soko lako. Kwa maoni ama ushauri wasiliana nami kwa email: lucymike2009@yahoo. com au simu na: 0713 331455
0 Michango:
Post a Comment