Jumla ya wanawake 187,267 wamefanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi huku 7,602 wakipatiwa matibabu katika mradi uliofadhiliwa na Taasisi ya Bill and Melinda Gates baada ya kukutwa na ugonjwa huo.
Mradi huo uliokuwapo kwa miaka mitano ulikuwa ukitekelezwa na taasisi za Marie Stopes Tanzania (MST), Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (Umati) na PSI.
Akizungumza wakati wa kufunga mradi huo juzi, Mkurugenzi Mkazi wa MST, Anil Tambay alisema idadi hiyo ya wanawake imetoka katika mikoa 22 ambako mradi huo ulikuwa ukitekelezwa.
“Mradi huu ulijikita kupunguza athari za saratani na shingo ya kizazi kwa wanawake, tumefanya uchunguzi na kutoa matibabu,” alisema Tambay.
Alifafanua kuwa wakati wa kuanza kwa mradi huo walitoa mafunzo na kupata watoa huduma 210 waliohudumia vituo 79 vilivyoanzishwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Afya ya Uzazi wa Wizara ya Afya, Dk Hussein Kidanto alisema asilimia 38 ya wagonjwa waliofika katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road mwaka 2015 walikuwa na saratani ya shingo ya kizazi.
0 Michango:
Post a Comment