UPO kwenye uhusiano wa kimapenzi na mtu ambaye humuelewi? Unahitaji kujua dhamira yake kwako kama ana malengo ya muda mrefu na wewe au kinyume chake? Ni rahisi sana kutanzua hilo. Makala haya yana jibu lililotimia.
Muda wako ni wa thamani kubwa, hivyo usikubali mtu auchezee. Weka kituo kwa mtu ambaye unathibitisha kabisa kuwa ameamua kuwa na wewe kwa maisha yake yote yaliyosalia. Siyo yule aliye macho juu, anayesaka sehemu ya kuweka nanga.
Je, wewe ni wa majaribio? Sasa kwa nini unamruhusu aingie kwenye historia yako wakati lengo lake ni kupita tu kwako? Yeye anafanya utafiti kujua mtu gani anayeweza kuendana naye, kwa hiyo anakuja kwako kukujaribu, baada ya muda anaangalia mwingine.
Inauma sana wakati wa kuachwa. Mtu ambaye umemkabidhi moyo wako na kumtegemea kwa maisha yako yote ya baadaye, anakugeuka na kuhamisha upendo kwa mwingine mwenye jinsi yako. Unajiuliza umepungukiwa nini hujui. Angalia usifike huko.
Siku zote unatakiwa uwe wa kwanza kupigania furaha yako. Hawezi kutokea mtu wa pembeni ambaye anaweza kulia kwa niaba yako. Marafiki wema watasikitika kwa ulichotendwa lakini hawawezi kuhisi machungu ndani ya moyo wako. Hutakiwi kulia.
Ameumbwa na akili kama ulivyo wewe, hivyo hapaswi kukuchezea. Unatakiwa umsome kabla hujamuingiza moyoni. Kumuondoa aliye ndani yako ni ngumu mara 70 kuliko kumzuia asiingie. Fungua mlango kwa mtu uliye na uhakika naye. Mwili wako siyo wa majaribio.
Watu wengi wapo kwenye mateso haya. Nimekuwa nikipigiwa simu na wasomaji wangu ambao hutaka niwape muongozo kuhusu wapenzi wao. Hawawaelewi hata kidogo. Nyoyo zao zinateseka kwa sababu ya kuwafikiria. Wanajiona wamekamatika. Hapa natoa ufumbuzi.
SIKU YA KWANZA
Unaweza kumjua mtu aliye mbele yako kama ana malengo na wewe tangu siku ya kwanza. Anapozungumza nawe kuhusu mapenzi, atakuwa muongo. Eneo ambalo anahitajika kutoa ufafanuzi wa kina, yeye atakujibu mkato, akimaanisha hataki maelezo mengi.
Hali hiyo itoshe kukufanya utambue kuwa ana uwalakini. Hilo anza kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo. Jinsi ya kulishughulikia siyo kumkataa siku ya kwanza ya mazungumzo yenu, bali ni kumpa muda aweze kufunguka maisha yake yote kwako. Mantiki ni kwamba hatakiwi kukuficha kitu.
Ni kosa kubwa kuingia kwenye mapenzi na mtu ambaye humjui. Hata hivyo, siyo rahisi kumfahamu kwa kila kitu siku ya kwanza. Hivyo, unapaswa kutuliza kichwa na uchambue mazungumzo yenu kwa kila nukta, sehemu yenye shaka, hakikisha inaondoka.
Ilishaelezwa kuwa mapenzi yanahitaji muda, kwa hiyo jipe nafasi ya kumchanganua vilivyo mtu ambaye yupo kwenye kipindi cha uangalizi. Kauli zake ziwe thabiti kwako. Maswali yako yote aweze kuyajibu kwa ufasaha. Hakikisha hubaki na kiulizo chochote. Kama bado kuna eneo unalitilia shaka, jipe muda zaidi.
BAADA YA MAPENZI KUCHANUA
Zingatia hili kuwa penzi lenye migogoro siku zote halichanui. Mantiki ya kueleza hivyo ni kwamba unatakiwa kupima uhusiano wako kama unakua au unazorota. Angalia muda wako uliotumia, je, zipo alama za kusogea mbele au mnazunguka pale pale?
Jawabu la swali hilo linaweza kukupa sababu ya kuendelea na mwenzi wako au kuachana naye. Wanasema heri nusu shari kuliko shari kamili, kwa hiyo unapogundua mapema kuwa hakuna dalili ya penzi kushamiri, ujue picha haziendi. Ng’atuka usingoje kulizwa.
Jambo ambalo unapaswa kuzingatia ni kuwa siku zote zuia moyo kuzama moja kwa moja. Nenda hatua kwa hatua. Mwenda pole hajikwai, hivyo utaweza kutembea salama ikiwa utakuwa mwangalifu. Wengi wanaojuta na kuona wamepoteza uelekeo ni wale waliovamia mambo kwa pupa.
HATAKI MAZUNGUMZO YA KUJENGA MAISHA
Mathalan, inawezekana wewe una hamu ya kupata mtoto na kwa sababu unajua yeye ndiye mwenzi wa maisha yako, unaamua kumshirikisha. Ikiwa mwenzio ana malengo chanya na wewe, hilo atalipokea kwa shangwe lakini kama hakutaki hawezi kukubali. Noa akili zako.
Ukweli ni kuwa sababu ya mtu kumkwepa mwenzi wake anapozungumzia kujenga maisha ni kuogopa dhamira yake mwenyewe. Hana mpango wa kutulia, sasa maisha ya kujenga pamoja ya kazi gani? Itakukereketa wewe lakini kwake ni sawa tu.
Anataka muendelee kutumiana kisha siku akifanikisha wake atulie huko na kukuacha wewe ukihangaika. Maumivu yakutawale kwa maana wewe ulidhani yeye ni wako wa maisha lakini kumbe mwenzako alikuwa na lake kichwani. Alikufanya wa kuzugia.
Mfano; Pricilla alikuwa kwenye mapenzi mazito na mwenzi wake Shauri. Hivi sasa penzi lao limegawanyika na wawili hao wapo vipande viwili kwa maana ya kila mmoja kivyake. Kwa Shauri, hilo ndilo alitaka lakini Pricilla ni mateso ya moyo.
Pricilla alitamani kuolewa na Shauri, kwa hiyo akaanza kuwekeza maisha yake kwa Shauri akiamini safari ya maisha yao ya uhusiano ingewapeleka kwenye ndoa. Ilikuwa bora achelewe kurudi nyumbani lakini ahakikishe anapita nyumbani kwa mpenzi wake anamfanyia usafi na kumpikia.
Shauri hakuchukulia hilo kama mapenzi ya kweli aliyonayo Pricilla kwake, badala yake alimuona mrembo huyo anajipendekeza. Akamsimanga, akamnyanyapaa. Hakumpa umuhimu, akawa macho juu, mwisho akamuona aliyedhani ndiye anamfaa na kumpa nafasi ya kwanza.
Katika uhusiano wao, mara kwa mara Pricilla aliomba akatambulishwe nyumbani kwa wazazi wa Shauri lakini hilo halikufanyika. Kila siku aliibua visingizio ambavyo vilifanya azma ya Pricilla isitimie. Siku alipompata mrembo mwingine, haraka sana alimtambulisha kwa wazazi.
Si jambo jema kumtesa mwenzako. Pricilla alikonda mno ilipofika wakati wa kuachwa. Ilimtesa kwa muda wake na mapenzi makubwa aliyowekeza kwa mtu ambaye hakuwa na malengo naye. Ilimtesa kuona kuwa mwanamke kama yeye ndiye amechukua nafasi ambayo yeye aliiwekea mbolea, akapalilia, akaipandia mbegu na kumwagilizia.
VIPI MCHAKATO WA NDOA?
Pengine mmeshakubaliana kuhusu kufunga ndoa lakini vipi michakato? Anaratibu mambo kwa roho safi au anajivuta? Maisha ya ndoa hutawaliwa na matarajio ya furaha, kwa hiyo mhusika hutekeleza ratiba zilizo mbele yake bila kusukumwa. Muogope sana mtu ambaye mnakubaliana jambo kwa ajili ya maisha yenu lakini hatekelezi mpaka akikumbushwa.
Ndoa ni ya watu wawili wanaopendana na wameamua kwa moyo safi kuishi pamoja. Hii ina maana kuwa utekelezaji wa mipango ya ndoa, inatakiwa ifanywe na kila upande kwa shauku kubwa. Anayetegea aangaliwe upya. Je, ana kasoro za kujisahau na uvivu au bado anajishauri?
Kufunga ndoa ni wito, je, mwenzi wako anao? Kama ni mvivu au ana kasoro za kujisahau, unaweza kumhimiza ili muweze kwenda kulingana na ratiba lakini kama anajishauri, ni vizuri nawe ukatafakari kama ni sahihi kuingia kwenye maisha ya ndoa na mtu ambaye hayupo tayari. Mtu anayejishauri kufunga ndoa na wewe, maana yake hayupo tayari, bado anajiuliza.
Itakuja kukusumbua baadaye atakapolazimisha muachane kwa sababu hana cha kupoteza. Hakupendi kwa dhati na hakuingia kwenye ndoa kwa moyo mmoja. Hakikisha kuwa uliye naye leo, anakuhitaji pengine kuliko wewe. Mwenda pole hajikwai, mapenzi yanahitaji muda, siyo kwenda kwa pupa.
TULIZA AKILI HAPA
Kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye hajakata shauri la kuyajenga maisha yake kuwa endelevu ni tatizo kubwa. Itakuumiza kichwa kuelewa msimamo wake, wakati mwenzako hata mshipa hautashtuka. Vema kulijua hilo na uanze kupambana kuanzia leo.
Namaanisha kuwa kabla ya kutafakari kama mwenzi wako ana malengo na wewe au kinyume chake, sharti ujue kuhusu dira ya maisha yake. Inawezekana hajawa tayari kuwa na mwenzi wa kudumu wa maisha yake, hivyo chukua hatua haraka iwezekanavyo.
Kama dira yake inasomeka, basi jambo la kufanyia kazi ni msimamo alionao kwako. Je, anataka muishie kuwa wapenzi tu au anakusudia kuingia na wewe kwenye ndoa? Nalo hilo ni jukumu ambalo unapaswa kufanyia kazi. Nakusisitiza uchukue hatua kulingana na matakwa yako.
Hana malengo ya kudumu na wewe, je nawe unapenda kupoteza muda? Vipi malengo yako kwake ni kuzugia au wewe umeshaanza safari ya kujenga maisha endelevu? Akili ipo kichwani kwa sababu haitakiwi baadaye ujute peke yako kwamba amekupotezea muda.
Kipimo kizuri cha awali kabisa kujua kuwa kama mwenzio ana malengo na wewe ni utambulisho. Je, anakutambulisha kwa familia yake? Ni kwa kiwango gani cha utambulisho? Inawezekana akakutambulisha, wewe ukadanganyika kumbe anakucheza shere.
Utambulisho wake ufanyie kazi. Je, ameshatambulisha wangapi kabla yako? Inawezekana familia yake imeshapokea wakwe wengi mpaka hawaoni uzito tena. Kuna familia nyingine zinalea vijana wao kwa misingi wanayoita ‘uzungu’ kwamba yupo huru kufanya chochote, wazazi hawajali.
Wazazi hawaoni kero kuletewa mtu leo wakiambiwa ni mkwe wao, baada ya miezi miwili wakaletewa mwingine tena. Aina hii ya watu ipo, kwa hiyo chambua mambo na uone wapi pa kushika. Usikimbie eti kwa sababu nyumbani kwao alishatambulisha watano, jiulize kwa nini hao aliachana nao?
Pengine wewe ndiye mwenye bahati baada ya kutofautiana na waliopita. Hawakuwa wake, ila wewe ndiye wa maisha yake. Hivyo, chekecha ubongo ili ujue hatima yako mapema.
Usijirahisi au kulainika mapema, matokeo yake ukachezewa, mwisho ukaachwa na kuingizwa kwenye kapu la waliotambulishwa na kupigwa chini.
Jambo lingine ni kuwa usikubali utambulisho uishie kwa marafiki. Uhusiano wako na yeye, unapaswa kuwa rasmi. Mpeleke kwa wazazi wako naye akupeleke kwao. Baada ya hatua hiyo, wekeni hoja mezani za maisha yenu baada ya urafiki na uchumba. Je, mnaelewana? Basi vizuri sana.
Ikiwa hakuna maelewano. Anakupiga chenga kukutambulisha kwa wazazi wake. Pengine ameshakutambulisha lakini anarukaruka kila unapofungua mazungumzo kuhusu hatima yenu. Hataki mjadili ndoa, anafurahia mazungumzo ya kujirusha na ngono. Huyo ishi naye kwa machale.
JAMBO MUHIMU KWAKO
Penda kujiona mtu nambari moja kwa ubora kwa sababu Mungu aliona una umuhimu ndiyo maana akakuumba. Linda thamani na heshima yako, usikubali mapenzi yakuondolee nguvu ambayo Mfalme wa Mbingu na Ardhi amekupa.
Ni rahisi kudharauliwa ikiwa utakuwa na mtu ambaye hana mapenzi ya dhati na wewe. Atakusaliti, watu watazungumza pembeni. Atakusema vibaya, ukipita mitaani utaonekana kituko. Mpenzi mwenye uelewa na anayekupenda kwa dhati, atakulinda mahali popote.
Hatakusaliti, ataishi ndani yako. Linalokuuma, litamtesa. Wasiokupenda atawachukia. Marafiki zako atawageuza ndugu. Kinyume chake ni kwamba mwenzi asiyekupenda kwa dhati, si ajabu akashiriki kukumaliza.
Mapenzi yana siri kubwa. Kila mmoja ana ugonjwa wake wa kupenda. Wengine wanawapenda wapenzi warefu, lakini kuna kundi ambalo huchanganyikiwa zaidi kwa wafupi. Pamoja na mchanganuo huo, kuachwa inauma hata kama anayekutosa hukuwa na mapenzi naye.
Ile dhana tu ya kuachwa ndiyo hutesa watu. Kuna dhana kwamba anayeacha mara nyingi hujiona mshindi dhidi ya aliyemuacha. Na hiyo ndiyo sababu ya wengi kuumia wanapofungiwa milango ya kukatisha uhusiano ambao pengine hata hawakuwa na masilahi nao.
Mathalan, mwanamke anaweza kuwa havutiwi na mtu aliyenaye kwa maana moja au nyingine. Ilitokea kuwa naye kama ajali tu! Kutokana na kutokuwa na hisia naye, hakuona tatizo kumsaliti kwa mwanaume mwingine, lakini huwezi kuamini siku akiambiwa basi, atalia machozi na kuomba msamaha.
Si kwamba atalia kwa sababu ya mapenzi ya dhati aliyonayo kwa mwenzi wake, kwamba inamuuma kuachana naye, ila kinachomtesa ni zile hisia za kuachwa. Na ingetokea kuwa yeye ndiye anayeamua kuacha, tafsiri ingekuwa kinyume chake.
Macho yangekuwa makavu na ikiwezekana angekwenda kusimulia kwa marafiki: “Aah, James nimempiga chini kanililia huyo!” Anafurahi dada yetu na wenzake watampongeza kwa kugongesheana viganja!
Tatizo kubwa ambalo linawagharimu wengi ni kuwa mapenzi yanabebwa kama aina ya mchezo wa kuigiza. Watu wanaingia kwenye uhusiano kwa kujaribu. Kuna waliofunga ndoa si kwa kuchaguana, isipokuwa walidanganyana kwa hisia za “mapozeo” mwisho wa siku wakazoeana, ikawa ngumu kuachana.
Wapo wanaoingia kwenye ndoa si kwa kuvutwa na nyoyo zao, ila wanakabiliwa na fikra za “waoaji wenyewe hawapo, acha nimkubali huyu huyu!” Mapenzi ni nguzo maalum mno kwa maisha ya binadamu, kwa hiyo ni vema yabebe heshima inayostahili.
Ogopa sana mtu anayekuwa na wewe kwa sababu haoni chaguo lake. Adhabu yako ni kubwa mbele ya safari ingawa unaweza kujiona upo kwenye bwawa la asali mwanzoni. Kiama chako ni pale atakapomuona anayedhani ndiye sahihi kwake. Utasilitiwa upende usipende!
Nimekuwa nikisisitiza hili kuwa ni bora kuacha kumsogelea kabisa kuliko kumdanganya unampenda wakati unamcheza shere. Ukatili wako ni mkubwa kwa maana yeye anaweza kudhani amefika na akatuliza ‘mizuka’ yote, hivyo akapandikiza matarajio juu yako.
Siku atakapojua haupo naye atajisikiaje? Unaweza kuua bila kukusudia kwa sababu binadamu tumeumbwa na roho tofauti. Utamuona aliyekunywa sumu kwa mapenzi ni mjinga kwa sababu hayajakufika. Kuna waliosema wao ni ngangari lakini ukurasa ulipofunguka kwao, waliona dunia chungu.
Kuna watu hawaoni hili umuhimu, mpenzi maana yake ni msiri wa maisha yako. Unapokuwa umelala fofofo hujitambui, ubavuni kwako yupo yeye. Anaweza kukufanya lolote wakati wewe unaogelea ndotoni. Mpende akupendaye, mchague mwenye malengo na wewe, vinginevyo utajuta.
0 Michango:
Post a Comment