Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Mhe. Freeman Mbowe amesema kuwa hali ya Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu
sasa imezidi kuimarika na kusema atasafirishwa kwa matibabu ya awamu ya tatu
siku za karibuni.
Mbowe
amesema hayo leo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu
ya chama hicho, alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya Tundu Lissu na kusema
mpaka sasa Mbunge huyo anaendelea vizuri na kudai amefanyiwa upasuaji mara
17.
"Tundu Lissu mpaka sasa amefanyiwa
upasuaji mara 17 amewekewa damu nyingi kuliko mgonjwa yoyote katika hospitali
ya Nairobi lakini Mungu ameendelea kutenda miujiza kwake, saizi mashine zote
zilizokuwa zinamsaidia zimeondolewa, saizi hapumulii mashine tena, mirija yote
aliyokuwa anatumia kwa ajili ya chakula imeondolewa na juzi kwa mara ya kwanza
aliweza kukaa" alisema
Mbowe
Mwenyekiti wa CHADEMA aliendelea kueleza kuwa "Matibabu
ya awamu ya tatu ya Tundu Lissu yatafanyika nje ya nchi haitakuwa tena Kenya wala
Tanzania, lakini kwa sababu za usalama hatuwezi kusema atakwenda sehemu gani au
nchi gani, ukifika wakati sahihi tutasema hiyo awamu ya tatu ya matibabu
itakuwa ya muda mrefu kidogo" alisema Mbowe
Mbali na hilo Mbowe ameendelea kusema kuwa serikali inafahamu
watu ambao wameshambulia Tundu Lissu na kudai wao hawana imani na vyombo vya
dola nchini na kusema vyombo hivyo vimekuwa tawi la Chama Cha Mapinduzi (CCM)
hivyo hawana nia ya dhati katika kufanya uchunguzi juu ya sakata la Tundu Lissu
kupigwa risasi mnamo Septemba 7, 2017.
0 Michango:
Post a Comment