Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,
Anna Mghwira amelitaka Jeshi la Polisi kuwa makini na madereva wa magari
yanayosafirisha magazeti akisema mara nyingi wamekuwa wakiendesha kwa mwendo
kasi.
Mghwira amesema hayo baada
ya kuwatembelea kuwajulia hali majeruhi wa ajali iliyotokea wilayani Mwanga
ikihusisha gari lililokuwa likisafirisha magazeti.
Katika ajali hiyo, ambayo
magari mawili yaligongana uso kwa uso watu wanne walijeruhiwa na wawili
wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kilimanjaro, Hamis Issah amesema ajali hiyo imesababishwa na mwendo kasi wa
dereva wa Toyota Hiace ambalo lilikuwa likisafirisha magazeti.
Amesema Hiace lililokuwa
likiendeshwa na Godfrey Malisa (37) lilihama njia na kugongana uso kwa uso na
Toyota Passo iliyokuwa ikiendeshwa na Ibrahim Mangi (38).
Kamanda Issah amesema katika
ajali hiyo iliyotokea jana Ijumaa saa 12:00 asubuhi, majeruhi mmoja mwanamke
amevunjika mguu wa kulia na dereva wa Hiace amevunjika mguu na ana maumivu
ya kiuno.
Majeruhi Jane Kanyika (31)
anayeendelea na matibabu KCMC amesema baada ya gari lao kugongwa lilisukumwa
umbali wa mita 100 kutoka barabarani.
Amesema alishtuka baada ya
kusikia kilio cha mtoto wake na kwamba wananchi walipofika eneo la tukio
kuwasaidia alibaini wanawe wawili walikuwa wamepoteza fahamu.
Kanyika amesema baada ya
hapo askari wa usalama barabarani walifika ndipo walipopelekwa Hospitali ya
Wilaya ya Mwanga na baadaye kuhamishiwa KCMC.
Dereva Mangi aliyepata
maumivu kifuani amesema alishangaa kuona Hiace ikimfuata upande wake na
alipojaribu kuikwepa aligongwa na kusukumwa hadi nje ya barabara.
0 Michango:
Post a Comment