John Bocco |
Na Mwandishi wetu
BAADA ya Klabu Bingwa ya
Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kuanza rasmi mazoezi jana jioni kujiandaa na
mchezo ujao dhidi ya Ndanda, daktari wa timu hiyo, Mwanandi Mwankemwa,
amezungumzia hali za kiafya za baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi.
Wachezaji wa Azam FC waliokuwa
majeruhi ni nahodha John Bocco ‘Adebayor’, Stephan Kingue waliopata majeraha ya
misuli ya paja kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
(VPL) dhidi ya Simba, ambao matajiri hao walishinda bao 1-0 lililofungwa na
Bocco.
Wengine wanaouguza majeraha,
ambao waliukosa mchezo huo ni kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, kipa Mwadini
Ally (nyama za paja) na beki Shomari Kapombe, ambaye ni mgonjwa lakini hivi
sasa akiendelea vema.
Akizungumza na mtandao rasmi
wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya jana,
Mwankemwa alisema kuwa Bocco na Kingue watakaa nje ya dimba kwa muda wa wiki
mbili tokea jana, huku Sure Boy akitarajiwa kuanza rasmi mazoezi leo na Mwadini
akipumzishwa kwa siku tatu kuanzia jana.
“Bocco hali yake inaonekana
kuimarika vizuri tokea alipopata majeraha hayo ya kuchana msuli wa nyuma ya
paja, Stephan (Kingue) kwa upande wake naye amechana msuli wa mbele ya paja,
hivyo wote watakaa nje ya dimba kwa muda wa wiki mbili kutoka sasa (jana) na
wataanza mazoezi mepesi baada ya wiki moja,” alisema.
Daktari huyo bingwa mzoefu, alisema hali za wachezaji
wengine ziko vizuri kabisa kuendelea na mikikimikiki ya maandalizi kuelekea
mechi zijazo za ligi pamoja na michuano mingine.
0 Michango:
Post a Comment