Wachimaji waliookolewa katika Mgondi wa RZ mkoani Geta wakipatiwa huduma ya kwanza baada ya kuokolewa |
Na Mwandishi wetu
WAKIWA wameloa tope la udongo
mwekundu wa mgodini uliokuwa umezifunika nguo zao, wachimbaji hawa 15,
hawakuamini macho yao baada ya kuliona tena jua kwa mara ya kwanza, kufuatia
kuwa chini ya ardhi, kwa siku nne mfululizo.
Miili yao haikuwa na nguvu, tumboni
hakukuwa na kitu na njaa ya siku nne ilikuwa imewatafuna vilivyo kiasi cha
kushindwa kusimama kwa miguu yao miwili baada ya kuokolewa.
Kwa wachimbaji hawa wa mgodi wa RZ
uliopo mkoani Geita, nafasi ya pili ya kuishi waliyopewa, itakuwa ni kumbukumbu
ambayo hawataisahau kamwe katika maisha yao.
Kutenganishwa na mazingira ya
kawaida ya dunia na kuwa chini ya kifusi cha mgodi ambako harufu ya kifo
ilianza kuwa dhahiri kwenye pua zao, ni mkasa utakaobaki daima vichwani mwao na
utakuwa kama mkanda wa video utakaojirudia kucheza vichwani mwao kwa miaka
mingi.
Baada ya zoezi la uokoaji,
wachimbaji wote 15 waliokolewa Jumapili hii (jana) katika mgodi huo wa dhahabu
uliopo Nyarugusu. Zoezi halikuwa rahisi katu na lilidumu kwa siku tatu.
Kwa wananchi wengi waliokuwa
wamekusanyika jirani na mgodi huo, tukio hilo lilikuwa kama filamu wakati
wakiwashuhudia wachimbaji hao wakitolewa mmoja baada ya mwingine.
Baadhi yao, wakiongea kwa tabu
walieleza kuwa, kukaa kwa siku nne kwenye kifusi hicho kuliwakatisha tamaa na
kuzishuhudia siku zao za kuishi duniani zikikiyoyoma kila mshale wa saa
ulivyokuwa ukitembea.
Na sasa wakiendelea kupatiwa
matibabu kwenye hospitali ya mkoani Geita, baada ya kupewa huduma ya kwanza
punde walipookolewa, wanaendelea kukusanya nguvu, na pale zitakapowaijia, bila
shaka watahitaji muda wa kutafakari mustakabali wao baada ya kukikwepa kifo,
katika shimo lenye udongo uso na huruma.
0 Michango:
Post a Comment