Na Mwandishi wetu
MAOFISA watano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
wanaotuhumiwa kushiriki kumwondoa faru John kutoka katika Creta hiyo
walikamatwa juzi kwa mahojiano ili kujua ukweli kuhusu mazingira ya kupotea
kwake.
Hatua ya maofisa hao kukamatwa imekuja siku tatu baada ya Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa kuituhumu menejimenti, wafanyakazi wa NCAA na Baraza la
Wafugaji (NPC) kuwa imejaa vitendo vya rushwa na wizi na asingeweza kuvumilia
sakata la faru John ambaye alisema kuwa aliuzwa kwa Sh200 milioni kwenye Hoteli
ya Grumet iliyo Hifadhi ya Serengeti na kuwa walipokea fedha za awali Sh100
milioni.
Waziri Mkuu alisema anataka kumwona faru huyo, nyaraka za
kumhamisha na kama amekufa basi apelekewe hata pembe ofisini kwa kuwa anajua pa
kuzipeleka.
Alisisitiza kuwa ikibainika kuna ambao wamekiuka taratibu
watawajibika.
Habari za uhakika kutoka Ngorongoro, ambazo zimethibitishwa na
Jeshi la Polisi zinasema kuwa maofisa hao watano wanashikiliwa katika kituo
chao cha Ngorongoro kutokana na ushiriki wao kwa njia moja au nyingine.
Wanaoshikiliwa ni pamoja na Israel Naman ambaye alikuwa Kaimu mkuu
wa idara ya uhifadhi wakati faru huyo akiondolewa.
Wengine ni Cuthbert Lemanya, ambaye alikuwa Mkuu wa Kanda ya
Creta, Dk Athanas Nyaki ambaye anadaiwa kumdunga sindano ya usingizi ili aweze
kubebwa.
Maofisa wengine waliokamatwa ni aliyekuwa Mkuu wa Idara ya
Maendeleo ya Jamii wa Mamlaka ya Ngorongoro, Kuya Sayaleli na aliyekuwa Kaimu
Mkuu wa Idara ya Ikolojia, Patrice Mattey.
Ofisa mmoja wa NCAA, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake jana
alisema maofisa hao walikamatwa juzi jioni na jana walikuwa wanaendelea
kuhojiwa.
“Tuiache serikali ifanye kazi kwani ni muhimu sana kujulikana
ukweli wa tukio hili,” alisema
ofisa huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo hakupatikana jana
kuelezea tukio la kukamatwa maofisa hao, baada ya simu yake kupokelewa na
msaidizi wake ambaye alieleza yupo kwenye kikao.
Lakini, ofisa wa mmoja wa polisi, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina
kwa kuwa si msemaji alikiri kukamatwa maofisa hao kwa mahojiano.
Chanzo cha sakata
Akiwa katika ziara ya kikazi Ngorongoro, Waziri Majaliwa aliibua
sakata la kuhamishwa kinyemela faru huyo na kudaiwa kupelekwa Grumet.
Waziri mkuu alitaka ukweli kuhusu upotevu wa John aliyeondolewa
Creta na kupelekwa Grumet na kudaiwa kufa huku taarifa za kifo hicho zikifanywa
siri.
Waziri Mkuu alitaka kupewa nyaraka zote zilizotumika kujadili
kumuondoa faru na kuamua kumpeleka Grumet.
Waziri Mkuu alitoa hadi Desemba 8 (jana) awe amepata taarifa zote,
ikiwamo ya daktari inayothibitisha kifo hicho na kwamba pembe za faru huyo
zifikishwe ofisini kwake. Pia, Majaliwa alisema ikibainika wapo waliokiuka
taratibu watawajibika.
BONYEZA HAPA KUTEMBELEA UKURASA WETU WA FACEBOOK
0 Michango:
Post a Comment