Mwandishi maalum
KITUO cha kukuza vipaji cha Green Sports Academy kutoka jijini
Nairobi, Kenya kinatarajia kufanya ziara maalumu kwenye makao makuu ya Klabu
Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC.
Ziara hiyo ya siku sita itakayoambatana na mechi za kirafiki,
itaaanza rasmi Desemba 20 jioni watakapowasili nchini hadi Desemba 25 mwaka huu
watakaporejea nchini kwao.
Green Sports itakuja nchini ikiwa na timu zake nne za umri tofauti
chini ya miaka 13, 15, 18 na 21, ambapo itacheza mechi tatu za kirafiki kuanzia
Desemba 22, 23 na 24 dhidi ya timu za vijana za Azam FC.
Uongozi wa kituo hicho kupitia kwa Mkurugenzi wa Ufundi, Stephen
Ochiel Otieno, umetoa shukrani zake za dhati kwa uongozi wa Azam FC kwa
kuwakubalia ziara hiyo ya kuja hapa nchini.
Otieno amesema kuwa hiyo itawahamasisha sana vijana wadogo wenye
vipaji kuelekea kuwa nyota wa kimataifa katika siku za usoni, huku pia kwa
upande wao wakiangalia mbele kuendeleza ushirikiano wa kudumu na Azam FC,
ambayo kwa sasa ndio klabu bora iliyowekeza kwa vijana katika ukanda huu.
Huu ni ugeni mkubwa wa pili kwa mwaka huu kwa Azam FC ikihusisha
kituo cha kukuza vipaji, wa mara ya kwanza ulikuwa ni mwezi Juni ilipozialika
timu mbili za Afrika Mashariki, Football For Good Academy ya Uganda na Ligi
Ndogo Academy ya Kenya kwenye michuano ya Azam Youth Cup 2016, ambayo pia
iliishirikisha Future Stars Academy ya Arusha na kushuhudiwa wenyeji Azam FC
Academy ikitwaa ubingwa wa michuano hiyo.
0 Michango:
Post a Comment