//
Ads

Kifo cha mkulima, Baba aitupia lawama Serikali na Polisi

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Dk. Stephen Kebwe akizungumza na waandishi wa habari
Na Mwandishi wetu
Baba  mzazi wa  mkulima  Fabian Bago (22)aliyefariki  dunia  jana katika  hospitali ya rufaa   mkoa  wa orogoro  baada  ya   kupata  kipigo kutoka  kwa  wafugaji  wa jamii  ya  kisukuma ameitupia lawama  ofisi  za mkuu  wa wilaya , mkuu wa  mkoa  na jeshi  la polisi  na  kuzihusisha  na  kifo cha  mwanaye.

Akiongea  na  waandishi wa habari  nje ya chumba  cha kuhifadhia  maiti  cha  hospitali  ya  rufaa  ya  mkoa wa Morogoro ,Alan Bago alisema  kuwa  amezihusisha ofisi  hizo  kutokana  na  kupuuza malalamiko  yao baina  ya  wakulima  na wafugaji  katika kijiji  cha Kolelo  kata  ya Kolelo tarafa  ya  Mvuha wilaya ya Morogoro  .

Bago  alisema kuwa kuchelewa  kwa  viongozi  hao  kufanya  utatuzi wa migogoro  hiyo kunachangia  kwa  kiasi  kikubwa  jamii   kutokwa  imani  nao  na hivyo  kupelekea kuchukua  sheria  mkononi.

Akizungumzia   hali  ya  kutosikilizwa kwa malalamiko yao  diwani   wa  kata  hiyo  ya  Kolelo Erigius Mbena  alisema  kuwa yeye  kwa  upande  wake analilalamikia jeshi  la  polisi mkoa  wa Morogoro kutotoa ushirikiano  wakaribu kwa  wakulima  na badala  yake  kukaa  upande  wa wafugaji .

“ kwa mfano leo  hii baba  wa marehemu analazimishwa  kusema  kuwa  marehemu alipigwa na mkulima   mwenzie  na sio mfugaji “alisema Diwani  huyo .

Alisema  kuwa  kulazimishwa  kwa  baba  huyo ni  dalili  tosha   kuwa  kuna  njama  ya  kuharibu ushahidi  dhidi  ya watuhumiwa .

Aidha alisema kuwa kufuatia kupuuzwa kwa malamiko hayo yeye akiwashirikisha wazee wa kijiji hicho wana mpango wa kuunda timu ya wazee na kwenda kumuona Rais Magufuli au Waziri Mkuu ili waweze kupata ufafanuzi wa matatizo yao.

Akielezea tukio hilo Mbena alisema, marehemu alifariki dunia Januari 3 saa 10 jioni, baada ya kupata kipigo januari mosi kutoka wafugaji wa jamii ya kisukuma wakati akiwa njiani kwenda kwenye sherehe ya harusi ya babu yake.

Alisema, marehemu huyo alikuwa na mwenzake aliyejulikana kwa jina la Japhet Banzi wakiendesha pikipiki walipishana na wasukuma hao wakawasikia wakiongea kilugha na baadae wakawavamia na kuanza kuwapiga kwa fimbo na mapanga.

Aidha alisema, matukio kama hayo yamekuwa yakitokea tangu mwezi wa 8 mwaka jana baada ya wafugaji kuvamia eneo hilo na kwamba mpaka sasa tayari kuna watu zaidi ya 28 wenye majeraha baada ya kupata vipigo kutoka kwa wafugaji hao.

“nimejitahidi kufikisha malalamiko hayo polisi lakini naishia kuwekwa ndani na baadae kutolewa kwa dhamana ya kujiwekea mwenyewe na siitwi tena kuendelea na kesi” alisema Diwani huyo.

Hata hivyo Mkuu wa mkoa wa Morogoro DK. Steven Kebwe alikana kuhusika na kuchangia kutokea kwa kifo hicho na kwamba jukumu la Serikali ni ulinzi na usalama na kupanga mipango ya mbalimbali inayoleta maendeleo.

Dk. Kebwe alisema, licha ya Serikali kuwa katika kuboresha mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuondoa migogoro ya wafugaji na wakulima lakini watu hao waliopigana hawakupigana eneo la mashamba bali barabarani labda ni kwa ajili ya ugomvi mwingine.

Naye Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Ulrich Matei alisema ugomvi huo haukuwa wa mtu kukamata ng’ombe wa wafugaji bali walipigana barabarani na kwamba kufuatia tukio hilo mpaka sasa watu watano wameshakamatwa.

Alisema pia wameshaongeza nguvu kwa kupeleka askari zaidi kwenye kata hiyo licha ya kuwa ofisi ya Kituo cha polisi kuwepo eneo hilo na inaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine waliohusika na tukio hilo.
Sambaza kwenye Google Plus

Kuhusu Anonymous

Hii ni Blog yenye jukumu la kukupasha habari za Mtanzania mwenye hali ya chini ambaye hajapata nafasi ya kutoa maoni yake.

0 Michango:

Post a Comment