Na Mwandishi wetu
JESHI la Polisi Mkoa wa
Arusha linamshikilia mkazi wa Olasiti, jijini Arusha, Hamisi Amani (17), kwa
tuhuma za kumuua mwenzake wakati wakigombea soda.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, tukio hilo
lilitokea Desemba 25, mwaka huu, saa mbili usiku katika eneo la Kwa Morombo.
Kamanda Mkumbo alimtaja
marehemu kuwa ni Novatus Tadei (26), mkazi wa Kwa Morombo na kwamba aliuawa kwa
kuchomwa kisu kifuani upande wa kushoto.
“Marehemu na mtuhumiwa
walikuwa wapishi kwenye kampuni inayojulikana kwa jina la ZZ Catering
inayomilikiwa na Bashiri Ally.
“Siku ya tukio, marehemu
pamoja na wafanyakazi wengine, akiwamo mtuhumiwa, baada ya kumaliza kazi
waliyokuwa wanafanya, walipanda gari lenye namba za usajili T 375 CHH, aina ya
Toyota Hiace wakirejea nyumbani.
“Wakiwa ndani ya gari
hilo, mtuhumiwa Hamis aligundua kuwa soda aliyokuwa ameiweka ndani ya begi
lake, haipo na kuanza kuhisi marehemu ndiye aliyeichukua.
“Kwa hiyo, ulizuka
ugomvi baina yao na kuanza kutukanana matusi. Wakati ugomvi huo ukiendelea,
mtuhumiwa alimkaba marehemu na kuchukua kisu wanachotumia kwenye shughuli zao
za mapishi kilichokuwa ndani ya vyombo na kumchoma kifuani.
“Baada ya kuchomwa kisu,
Tadei alianguka chini na jitihada za wafanyakazi wenzake waliokuwamo ndani ya
gari hilo kuokoa maisha yake zilishindikana, kwani alifariki wakati anapelekwa
hospitali kwa ajili ya matibabu,” alisema Kamanda Mkumbo.
Alisema mwili wa
marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru na
mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi kukamilika.
0 Michango:
Post a Comment