Wanafunzi 229 wanasoma chini ya miti kutokana na uhaba wa Madarasa
Wanafunzi 229 wa Shule ya Msingi Mitambo wilayani Mtwara wanasoma wakiwa chini ya miti kutokana na uhaba wa madarasa matano.
Wanafunzi wanaosoma wakiwa chini ya miti ni wa darasa la tatu, nne, tano na sita.
Akizungumza na MCL Digital, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Rashidi Chalilo amesema wanafunzi hao ni kati ya 436 wa shule hiyo.
Chalilo amesema wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili kutokana na kuhitaji uangalizi zaidi wanasoma darasani pamoja na wa darasa la saba wanaojiandaa kwa mitihani.
Amesema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2009 ikiwa na wanafunzi 99 na sasa wapo 436 ikiwa na madarasa matatu pekee.
Mwalimu mkuu huyo amesema wazazi walijenga madarasa ya muda kwa kutumia miti na udongo na kuyaezeka kwa nyasi lakini baadaye yalibomolewa kwa maelekezo ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ili kupisha ujenzi wa madarasa ya kudumu.
Akizungumzia suala hilo, kaimu ofisa mtendaji wa Kijiji cha Mitambo, Ally Mselemu amesema wanasubiri kupelekewa saruji na vifaa vingine vya ujenzi.
“Wananchi tuko tayari kujitolea nguvu kazi kuboresha shule yetu, hivyo tunaiomba Serikali ituletee vifaa,” amesema Mselemu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Omari Kipanga amesema wameshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matatu pamoja na nyumba ya mwalimu.
Amesema Sh156 milioni zimetengwa kutoka katika mfuko wa elimu ambazo zinatokana na mapato ya korosho.
Kipanga amesema mfuko wa P4R pia umeidhinisha Sh326 milioni kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu katika halmashauri hiyo.
0 Michango:
Post a Comment