Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu |
SAKATA la Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) kuweka fedha katika akaunti maalumu kwenye benki za
biashara limechukua sura mpya baada ya Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT),
Profesa Benno Ndulu kusema si kosa kisheria.
Profesa Ndulu, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa
Bodi ya TRA iliyovunjwa na Rais John Magufuli Jumapili iliyopita, alisema mjini
Arusa jana kuwa hakuna hasara kiuchumi kuweka fedha kwenye akaunti maalum
isipokuwa hilo suala lilikuwa na hali nyingine.
Japokuwa Profesa Ndulu hakutaka kufafanua zaidi
kwa maelezo lilichomekewa tu katika mkutano na waandishi wa habari wa kuelezea
hali ya uchumi, alisema hali hiyo ndiyo suala lililozungumzwa na siyo kusema
“fixed deposit account” ni mbaya.
“Kwani amesema fixed account zote ni mbaya,
pamoja na za watu binafsi? Ndo hivyo sasa. Nilijua mtachomekea hilo kwa hiyo
nilikuwa tayari,” alisema mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam.
Profesa Ndulu alisema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa
habari walipotaka kujua athari za kiuchumi kwa taasisi za umma kuweka fedha
kwenye akaunti maalumu tena benki binafsi.
Kauli hii ya Profesa Ndulu imekuja siku moja baada ya Rais
Magufuli kueleza kilichochangia kuchukua uamuzi wa kutengua uteuzi wa Mwenyekiti
wa Bodi, Bernard Mchomvu na pia kuivunja bodi yake iliyokuwa na wajumbe tisa.
Kati ya wajumbe hao tisa, watano wanaingia kwa mujibu wa sheria na wanne ni wa
kuteuliwa.
Wajumbe wanaoingia kwenye Bodi kwa mujibu wa sheria ni Gavana wa
BoT, Profesa Beno Ndulu; Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata; Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha wa Jamhuri ya Muungano, Doto James; Katibu Mkuu Wizara ya Fedha
Zanzibar, Khamis Mussa Khamis; na Katibu Mkuu Mipango. Bodi hiyo ilivunjwa
Jumapili iliyopita.
Rais Magufuli alisema juzi kuwa Bodi ya TRA iliyokuwa na watendaji
hao wakuu wa idara na taasisi za Serikali ilifanya dhambi ya kuidhinisha uamuzi
wa menejimenti kuweka mabilioni ya shilingi katika benki za binafsi.
“Juzi hapa tumekuta Sh26 bilioni
zilizokuwa zimetolewa TRA kwa ajili ya matumizi ya TRA zikapelekwa kwenye
mabenki matatu kama ‘fixed deposit account’ na bodi ikapitisha. Ndiyo maana
nilipozipata hizo hela; hela nikazichukua na bodi kwaheri,” alisema Rais Magufuli alipokuwa mgeni
rasmi kwenye mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)
yaliyofanyika mjini Kibaha mkoani Pwani ambako jumla ya watu 4038 walihitimu
shahada mbalimbali
Ukwasi wa mabenki
Katika hatua nyingine Profesa Ndulu amesema ukwasi wa fedha katika
mabenki umeshuka ikilinganishwa na kipindi cha nyuma hatua inayotatiza utoaji
wa mikopo ya muda mrefu kwa ajili ya uwekezaji nchini.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mara baada ya kufungwa
mkutano wa 18 wa taasisi za fedha uliofanyika kwa siku mbili jijini Arusha
alisema hali hiyo inafanyiwa kazi na wadau wa taasisi hizo ili kuja na mbinu
kufanya kuwa endelevu kwani uchumi unategemea uwekezaji unaotegemea mikopo ya
muda mrefu.
Profesa Ndulu alisema BoT itahakikisha inaziwezesha benki
kuendelea na jukumu lao la kutoa mikopo pia kuwa wabunifu wa kutafuta pesa kwa
ajli ya amana badala ya kutegemea Serikali pekee.
“Benki zinaweza kukusanya amana kwa
kiwango kikubwa lakini kama nilivyosema jana (juzi) kuwa katika kila Sh60 kati
ya Sh100 zipo kwenye mikono ya watu badala ya kuwekwa akiba benki hivyo ni
muhimu zikawekwa mbinu ya kuzipata kwa ajili ya kuwawezesha wawekezaji
kuzitumia kwenye uzalishaji,”alisema.
Alisema katika kufanikisha mpango huo lazima kuvutia mitaji kutoka
nje kwani hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kupiga hatua kwa kutegemea fedha
za maendeleo na uwekezaji zitokane na mapato ya ndani pekee akitolea mfano wa
China kuwa ni mfano uchumi wake kutegemea mitaji inayotoka nje ya nchi hiyo.
Katika hatua nyingine Profesa Ndulu alisema amekubaliana na wadau
wa sekta ya fedha kuongeza nguvu katika kutoa mikopo na kuboresha mifumo ya
taarifa kwa wale wanaotaka mikopo kwa ajili ya kilimo katika mnyororo mzima wa
thamani kuanzia uzalishaji hadi kufika kwenye soko.
Profesa Ndulu alisema Tanzania imekaa vizuri kijiografia kufanya
biashara na nchi zisizo na bahari zikiwemo Malawi, Uganda, DRC na Zambia katika
kuwezesha sekta ya fedha kusaidia eneo la usafirishaji, bandari kufanya kazi na
huduma kutolewa inavyotakiwa.
Mwenyekiti wa wenye mabenki ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya
CRDB, Dk Charles Kimei amesema waendeshaji wa mabenki wamenufaika na kuelewa
mikakati na fursa za Serikali ambayo itawawezesha wao kutoa fedha kwa
wafanyabishara.
Alisema wao kama CRDB wameweza kukusanya amana za Sh500 bilioni
zinazokopeshwa kwa wafanyabiashara katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na
kufungua matawi madogo madogo 100 nchi nzima.
Dk Kimei alisema serikali inapobanwa kifedha kutokana na kutegemea
mashirika ya umma inawapa fursa sekta binafsi kupanua wigo wao kuwafikia
wananchi wengi.
0 Michango:
Post a Comment