VIJANA wa Kanda ya Ziwa mpo tayariii? Hii ni habari njema kwenu kwani Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imepanga kuendesha msako wa vipaji kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 ‘U-17’ Jumamosi ijayo Novemba 26, mwaka huu ndani ya Uwanja wa CCM, Kirumba Mwanza.
Mpango huo wa kitaifa wa mabingwa hao uliopita kwenye mikoa mingine mitano nchini, utafanyika kuanzia saa 1.00 asubuhi hadi 9.00 Alasiri ndani ya jiji hilo lenye historia ya kutoa wachezaji wengi wenye vipaji waliowahi kutamba na wengine wakitamba hivi sasa nchini.
Mara ya mwisho zoezi hilo lilifanyika jijini Mbeya na kuhudhuriwa na vijana 433, ambapo Azam FC ilivuna vijana 10 pekee watakaoingia kwenye mchujo wa mwisho utakaofanyika mwezi ujao kwenye makao makuu ya Azam Complex, Chamazi.
Mpaka sasa kwenye mikoa yote hiyo mitano, Dar es Salaam, Tanga, Morogoro & Dodoma, Visiwani Zanzibar na Mbeya, Azam FC imechagua jumla ya vijana 60 kati ya vijana 2,999 waliofanyiwa usajili.
Kwa majaribio mengine ya wazi katika maeneo mengine kuzunguka Tanzania yatatangazwa hivi karibuni.
0 Michango:
Post a Comment