OFISA Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba amewaomba Watanzania kutumia kampuni hiyo kwa mawasiliano kwa kuwa hivi sasa huduma zake zimeboreshwa.
Kindamba aliyasema hayo jana wakati wa akitiliana saini makubaliano ya matumizi ya mawasiliano na mtandao wa TTCL na Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo (SUA) kwenye hafla fupi iliyofanyika chuoni hapo.
Amesema licha ya kwamba historia ya kampuni haikuwa njema zamani na kufanya wateja kukosa huduma ipasavyo na hivyo kuamua kuhama lakini kwa sasa hali imebadilika.
“Historia haikuwa njema nyuma kwa TTCL , mtu akipiga simu ilikuwa anapatiwa huduma baada ya wiki mbili hadi tatu, lakini kwa sasa hali imebadilika” alisema Kindamba.
Aidha, Kindamba aliwapongeza SUA kwa kuchukua hatua ya kurejea TTCL kwa mawasiliano na kuahidi kutowaangusha katika utendaji kazi wao na kufanya huduma walizoanza kuzifurahia kuwa endelevu.
Hata hivyo, amesema kuwa TTCL inatarajia kuwa na kasi ya 3G na 4G baada ya wiki moja itakayosaidia kuboresha huduma na kuwezesha upatikanaji wa huduma za TTCL mobile yenye kasi zaidi.
Awali Makamu Mkuu wa Chuo kikuu (SUA) Profesa, Raphael Chipunde amesema kuwa SUA imeamua kuingia mkataba na TTCL baada ya kubaini mabadiliko makubwa yaliyopo kwa TTCL kwa sasa juu ya utoaji wa huduma zao.
Amesema walifikia makubaliano na kuandaa mkataba ambao utaweka chuo katika huduma nzuri itakayowezesha chuo kuendelea kufanya kazi bila matatizo.
“Naweza kusema kwamba Intanet ndiyo imeshika damu kwenye mwili wa binadamu kwa sasa, hivyo bila Intanet ya uhakika chuo kitayumba” amesema,” amesema Profesa Chipunda.
Aidha, amesema kuwa wameamua kuweka makubaliano hayo licha ya kuwa ni ya sehemu ya SUA huku wakiendelea kutumia kampuni nyingine ambayo hakutaka kuitaja na kwamba wakiona TTCL ipo vizuri watahamia kwa asilimia 100.
0 Michango:
Post a Comment