Mpokee na umkarimu aliyetoka kutendwa na mwenzi wake aliyempenda sana, kisha umsaidie kuhamisha maumivu aliyokuwa nayo yatoke kwake yaje kwako.
Mapenzi yana tabia mbaya sana! Kipimo chake kimapenzi siyo upendo wako kwake wala jinsi unavyomuonesha uhusika bora wa kimapenzi. Kipimo ni utashi wa moyo wake.
Je, amekupenda na kuridhia kuwa na wewe? Au ulimpata katika kipindi ambacho alikuwa na masumbuko ya moyo baada ya kutendwa?
Alikupenda au alitua kwako baada ya kuponyokwa na hifadhi aliyoitarajia? Je, alikukaribisha na kukuingiza moyoni au alikwambia “sawa” baada ya aliyemwamini kumtenda ndivyo sivyo?
Chukua hii; Mapenzi huongozwa na moyo. Na kwa kawaida moyo hujielekeza kwa mtu na kujifikisha ‘mazima’. Wakati mwingine hujielekeza na kujifikisha bila kupokelewa. Matokeo yake unakuwa unaonekana unalazimisha mapenzi. Mwenye kupendwa hataki!
Moyo wa binadamu una king’ang’anizi cha ajabu. Jinsi mtu anavyotendwa, ndivyo anavyozidi kuumia na kulihitaji zaidi penzi la anayemtenda.
Ona moyo wa binadamu usivyo na shukurani; Wakati akilalamika kutendwa, pale alipo kuna mtu anayemwonesha mapenzi yote ya ndani ya moyo. Anapewa zawadi na kupelekwa maeneo mazuri yenye mandhari ya kimapenzi lakini haiwi liwazo.
Pokea hii; Usimlaumu mtu asiyekupenda pamoja na upendo wote unaomuonesha. Huwezi kujua ndani yake kuna maumivu kiasi gani juu ya yule anayempenda lakini hapati anachokitaka. Siyo yeye, ndivyo moyo wa binadamu ulivyo.
Tatizo ni moja, moyo wa binadamu haukuumbwa na macho. Haumuoni anayestahili kupendwa na ambaye hastahili. Moyo ukishampokea mtu na kumkubali, yanakuwa mateso makubwa kwa mwenye moyo. Moyo una tabia ya kulazimisha matakwa yake hata kama hayawezekani.
Mtu anaweza kukuonesha dalili zote za kukukataa. Akakufanyia vitimbi vya kila aina. Akakusimanga na kukupeleka kwenye jumba la maonesho ya mabwege kama siyo mazuzu wa mapenzi. Pamoja na yote hayo, moyo unakushinikiza kuwa na huyohuyo anayekutesa.
Binadamu ameumbwa na macho, kwa hiyo anamuona anayefaa na asiyefaa lakini moyo hauna macho ndiyo maana hung’ang’aniza. Binadamu huchoshwa na mateso ya mapenzi na kukata shauri la kufanya mabadiliko lakini moyo huyakataa mabadiliko hayo.
Mtu katili ni yule anayemtesa mwenzake na kumwambia maneno makali: “Wewe mbona king’ang’anizi? Nimeshakwambia sikutaki.”
Anashindwa kuelewa kuwa huyo ni binadamu mwenzake, ana moyo kama yeye. Na tatizo siyo yeye, ni moyo ambao siku zote umekaa kihafidhina. Moyo haupendi mabadiliko!
Anayetamka maneno makali kama hayo, anajisahaulisha kwa sababu naye kwa wakati wake aliwahi kukumbana na kibano cha kumpenda asiyempenda. Na kama hayajamfika, naye ipo siku yake. Ahadi hiyo ni kwa sababu naye ana moyo na tabia za moyo duniani kote zinafanana. Avute subira!
Mtu mjinga ni yule anamyemcheka mwenzake anayebembeleza mapenzi. Anampigia magoti ampendaye, anaomba msamaha hata kama ni yeye aliyekosewa. Ni mjinga kwa sababu hajui kuwa mwenzake ana moyo ambao ukitaka lake ni lazima litimie.
Hata huyo anayemcheka mwenzake, siku ikimdondokea ataona matokeo. Anaweza kupitisha usiku mzima bila kupata japo usingizi wa mang’amng’amu. Siku itapita na asiwe na hamu ya kuingiza chochote tumboni. Kwa vile ana moyo, basi na asubiri.
Binadamu kama angeweza kuishi bila moyo, maisha yake yangekuwa mazuri mno. Maumivu ya mapenzi yasingekuwepo. Ingekuwa watu wakiachana, mmoja anasema “poa” na mwenzake anajibu “poa”, kisha kila mtu anashika hamsini zake. Kusingekuwa na kung’ang’aniana wala kupigiana simu usiku wa manane na kuombana misamaha.
Shida kubwa ni kuwa binadamu hawezi kuishi bila moyo. Moyo ndiyo injini ya mwili wa binadamu. Bila moyo hakuna maisha. Tuzingatie pia kuwa moyo ndiyo husababisha upendo wa dhati uwepo. Mgogoro unaletwa na wapendao kwa wapendwao.
MAPENZI YANATAKA UELEWA
Utampenda sana mtu, kwa bahati mbaya yeye anakuwa anampenda mwingine ambaye anamuumiza. Usipokuwa mwelewa, utajikuta unaumia kila siku. Yaani yeye anaumizwa na anayempenda kisha anakuumiza wewe ambaye huambiwi kitu kwa jinsi unavyompenda.
Lazima kufahamu kuwa mapenzi ya kweli hayakatishwi mara moja. Wewe mwenyewe ukipenda mahali kwa viwango vya kweli vya kupenda, ukikatishwa hutakuwa sawa. Utaumia mno!
Hivyo mwelewe mwenzako kuwa anashinikizwa na moyo wake. Usiseme: “Mimi nakujali na kukuonesha mapenzi yote, wewe unamng’ang’ania mtu wako.” Hizo ni kauli za kumuongezea maumivu. Zaidi uking’ang’ania, mtakosa wote. Wewe utamkosa yeye, naye atamkosa anayempenda.”
Kama kweli unampenda, msaidie aachane na huyo anayemtesa kwa utaratibu. Kuwa sehemu ya maumivu yake, labda mbeleni ukawa tiba yake, kisha moyo wake ukakupokea.
Amini kuwa moyo na hulka zake, huyo anayeng’ang’ania, siku akichushwa, yaani moyo ukisema basi, ndipo utaona kimya. Yuleyule aliyekuwa anapendwa anaweza kurudi kubembeleza na asipokelewe. Moyo wa binadamu ukishahama ni vigumu kurudi nyuma.
Moyo wa binadamu ukishageuka, kurudia mapenzi huwa sawa na mtu kubeba punda mkubwa begani. Wanaorudiana mara nyingi ni wale waliokuwa wanapendana ila wakawa wanajishaua na kudenguliana. Waliokataana kutoka moyoni huwa hawakaribishani tena.
MAPENZI HAYATAKI MASHINDANO
Nimeshaeleza kwa upana kuhusu moyo wa binadamu unavyofanya kazi na ubishi wake wa kuhamisha mapenzi. Hivyo basi, ni vizuri kwako kutambua hali halisi na kushika njia ambayo inakubalika.
Ni ukweli kuwa haiwezekani ukawa na amani pale unayempenda na kumfanyia kila unaloona ni zuri lakini yeye akawa hajali, na badala yake umakini wake wote anauelekeza kwa mtu mwingine.
Na asili ya moyo wa binadamu, humlazimisha mtu kutamani kupokea zaidi ya anachotoa. Siyo kwa maana ya zawadi kuwa akikupa simu, anakuwa anatarajia kupokea televisheni, la hasha!
Anayetoa anaweza kuelewa kabisa kuwa mwenzi wake hana uwezo wa kutoa vitu vikubwa. Ila anakuwa anahitaji kupewa shukurani za kimatendo kuliko maneno.
Mtu ambaye anashukuru kwa mazuri anayofanyiwa hujulikana. Ile hali ya unyenyekevu ambayo mtu anayepewa kitu huionesha, ndivyo ambavyo hutakiwa kuonekana kwa wapenzi, aliyepewa kwa aliyempa.
Hata hivyo, tabia ya kutaka kupokea kadiri anavyotoa ndiyo huzalisha malumbano na maumivu ya upande mmoja. Mapenzi yanahitaji uvumilivu hasa wakati wa kutoa, maana sivyo utakavyopokea.
Suala la kutoa na kupokea halipo kwenye vitu vya kuonekana, lina rangi nyingi. Mfano, unaweza kuwa unampigia sana simu mwenzi wako lakini yeye hakupigii. Na ukipiga, unaweza kukuta anaongea na mtu mwingine kwa muda mrefu.
Anaweza kukuomba umtumie muda wa maongezi na ukafanya hivyo lakini asikupigie hata mara moja. Ukimtumia SMS, anaweza kukujibu kwa kujisikia. Hali hiyo inaumiza lakini haipaswi kuutesa moyo wako.
Tambua kuwa ninyi wote mna jukumu la kupigiana simu na siyo lazima nani aanze. Usiseme: “Yaani kila siku lazima nianze mimi kukupigia.” Mapenzi hayajengwi kwa mashindano. Ukiliweka hilo kichwani litakuumiza zaidi.
Unaweza kuwa mshindi kwenye mapenzi na usiumie, endapo utasema na nafsi yako: “Mwenzangu ni mzito kupiga simu, sasa mimi nitampigia kila wakati.” Kisha ukajiwekea utaratibu wa kumzindua kwa kumpigia mara kwa mara.
Wewe ni mwepesi kumsifu mwenzi wako kwa mambo mbalimbali lakini yeye hafanyi hivyo. Usikasirike na kuacha! Mathalan kumwambia amependeza au anafanya vizuri kazi zake.
Ajabu ya moyo ni kuwa wakati wewe unamwambia amependeza kisha anaishia tu kusema “asante” au “uzuri nao unachangia”, kisha hakwambii hata mara moja, naye akikutana na mtu fulani anammwagia sifa kemkemu za kupendeza na uhodari wa kazi lakini anaishia tu kushushuliwa au kusemwa pembeni kuwa anajigonga!.
Hata wewe, yupo ambaye hukupongeza kwa kazi nzuri na jinsi unavyopendeza lakini humjali. Utashangaa kuwa huyo anayekupa sifa nyingi, naye hupewa na mtu mwingine lakini hajawahi kuzingatia hata mara moja. Moyo haujawahi kupewa mtihani ukafaulu. Moyo una rekodi ya kufeli tu!
SASA TUKUBALIANE
Mapenzi yana tabia mbaya mno. Unaweza kumhangaikia mtu ambaye anahangaika na mwingine. Anayekuumiza, kumbe yupo anaumizwa na mwingine.
Huwezi kujua moyo wake unatatizika na nini wakati wewe unalalamika anakuumiza. Pengine yeye anaumia zaidi.
Mwenzi wako anaweza kuwa karibu na wewe, mnazungumza kwa ukaribu kabisa, lakini akawa anakutesa vilevile.
Akawa anakupa muda wake wote, mnalala kitanda kimoja na bado akakutesa. Ni kwamba mapenzi yanapatikana moyoni. Utakuwa naye kimwili lakini moyo wake upo kwa mwingine ambaye naye pengine muda muda huo amelala na mwingine.
Kwa ukaribu ambao mtakuwa nao, utapenda akuhudumie lakini hutapata huduma ambazo ungependa upewe na mwenzi wako. Ni kwamba hamu ya utoaji huduma inatoka moyoni, nawe kwa wakati huo moyoni mwake haumo.
Mtu anaweza kutoka kuumizwa na mtu, akaachwa vibaya lakini baadaye akaanzisha uhusiano mwingine ambao utaisha kwa kumuumiza mwenzake. Huo ndiyo ukatili wa mapenzi!
Unadhani aliyeumizwa kisha akaumiza anastahili lawama? Hapana hata kidogo! Siyo yeye, ni moyo. Moyo hauna macho, hauoni penye mapenzi ya kweli. Upofu wa moyo ndiyo unaosababisha mapenzi yawe na tabia mbaya.
Kila siku omba Mungu akufunulie mwenzi wa kweli na umtambue. Usije kabisa kuamini moyo. Maana moyo wenyewe haujielewi. Unajiendeaendea tu! Moyo umenyimwa macho, basi imekuwa shida kubwa katika mapenzi.
0 Michango:
Post a Comment