//
Ads

Ujauzito ulivyoharibu ndoto za mwanafunzi wa darasa la tatu

Makutano yetu yalikuwa ni vichakani na alikuwa akinisubiri nikienda mashine kusaga na wakati nikitoka shuleni jioni
ndipo aliponilazimisha, nimekutana naye mara nyingi tu.”
Ni kauli ya mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13 wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Makutano wilayani Kilombero Mkoa Morogoro, ambaye sasa ana ujauzito wa miezi saba.
Binti huyo anasimulia mkasa huo kwa mwandishi wa makala haya baada ya kumbembelezwa kwa zaidi ya nusu saa amtaje
mhusika na mazingira yaliyosababisha kupata ujauzito huo.
Inaelezwa kuwa siku moja baada ya binti huyo kufika nyumbani kwao anakoishi na wazazi wake katika Kitongoji cha Igole Kijiji
cha Makutano wilayani Kilombero alianza kububujikwa na machozi bila kueleza kili-chompata.Inaendelea uk 24
Baada ya kupata taarifa hiyo ilimlazimu mwandishi kufunga safari kwenda kuonana na binti huyo.
Ni umbali wa zaidi ya kilometa 110 kutoka makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero mpaka kufika Kitongoji cha Igole. Mwandishi alitumia zaidi ya saa kumi mpaka kufika katika kitongoji hicho katika Kijiji cha Makutano anakoishi binti huyo ambaye jina lake linahifadhiwa.
Kutoka barabara kuu mpaka kitongojini ni zaidi ya kilomita saba umbali wanaotumia wanafunzi wa kitongoji hicho kwenda Shule ya Msingi Makutano kila siku. Hivyo kutembea kilomita 14 kwenda na kurudi kila siku.
Baada ya kuwasili nyumbani kwa binti huyo, ilimbidi mwandishi kutumia uzoefu wake wa kazi na kama mzazi kumshawishi binti huyo kuzungumzia suala hilo kwani hakutaka kuliweka wazi.
Baadaye binti huyo ambaye ni wa pili kuzaliwa katika familia yao, anasema kuwa baada ya kujenga mazoea ya muda mrefu na kijana anayedaiwa kumpa ujauzito, wakaanza uhusiano wa kimapenzi na kukutana naye mara kadhaa, hata alipopata ujauzito hakuweza kujigundua hadi zoezi la upimaji mimba lilipofanyika shuleni ndipo akabainika kuwa ni mjamzito.
Anaeleza kuwa alianza urafiki na kijana huyo kutokana na kupewa lifti ya pikipiki mara kwa mara wakati anakwenda shuleni.
Akisimulia hali yake ya afya, binti huyo anasema kuwa hivi sasa anakabiliwa zaidi na maradhi ya mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kupungukiwa damu na kwamba kila mara anapokwenda kliniki amekuwa akishauriwa kula mboga za majani ili kuongeza damu mwilini.
Mama Mlezi
“Sikuwa naelewa kuwa amevunja ungo kwani nilijua bado mdogo, nilikuja kushangaa tulipoitwa shuleni na kuambiwa mtoto wetu ni mjamzito, naimani usiri wa mtoto wangu umechangia kwani angenieleza kuwa alishakuwa mkubwa ningeweza kumwelekeza,” anasema Jasmin Liganga, mama mlezi.
Anaongeza kuwa alianza kukaa na mtoto huo tangu akiwa na miaka tisa na kwamba binti yake hivi sasa ameanza kwenda kliniki na kila wakati anaambiwa kuwa anaupungufu wa damu. Pia, wataalamu wamewaeleza kuwa wanatakiwa kuwa karibu na hospitali.
“Sasa hivi kliniki tunaenda wote maana na mimi ni mjamzito kama unavyoniona, tunachoomba hapa ni msaada tu wa Serikali (polisi) kukamatwa kwa mhusika aliyempa mimba mtoto wetu kwani ametoroka,” anasema.
Baba mzazi
Baba mzazi, Lenifred Mlimandola anasema anachotaka ni kuchukuliwa hatua kwa kijana aliyempa mimba mtoto wake.
Anasema alitoa taarifa polisi na mzazi wa kijana aliitwa na kueleza kuwa angetoa ushirikiano, lakini kitu cha kushangaza baba wa kijana huyo kutozungumza nae tena hata wanapokutana njiani kama vile wanaugomvi.
Mlimandola anasema kutokamatwa kwa kijana huyo kunaendelea kumpa wasiwasi kuwa mzazi wa kijana atakuwa anafahamu mtoto wake alipo kwani amekuwa haonyeshi ushirikiano wowote kwake na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.
Mwalimu mkuu
Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Makutano, Fabian Undole anasema kuwa mwanafunzi huyo aliyepata ujauzito anaonekana kuwa na umri mkubwa kwa sababu alianza darasa la kwanza akiwa na miaka 10.
Pia, anasema wanafunzi wawili walibainika kuwa wana ujauzito baada ya kupimwa shuleni hapo mwaka jana.
“ Ni vyema jamii ikabadilika na kuwathamini wanafunzi wa kike na kuona kuwa mtoto wa mwenzio ni wako na si vinginevyo,” anasema.
Mashirika yanasemaje
Mkurugenzi wa asasi isiyokuwa ya kiserikali la Young Strong Mothers Foundation inayosaidia wasichana wanaopata mimba wakiwa shuleni, Jackie Bomboma anasema ujauzito ni janga ambalo limekuwa likiwafanya watoto wa kike kukatisha ndoto zao wakiwa bado wadogo.
Bomboma anasema naye alipitia hali hiyo ndiyo maana anamsukumo wa kuwasaidia mabinti waliopata ujauzito huku akiamini kuna sababu nyingi zilizowasababisha kuingia kwenye janga hilo ikiwemo umbali wa kufuata elimu na utoro.
Anasema asasi yake bado inakumbana na changamoto ya kupatikana kwa ufadhili wa kuwakwamua mabinti wanaojifungua wakiwa wadogo jambo linalochangia hali ya unyanyapaa wanayokutana nayo kutoka kwa jamii kuendelea.
Aidha, anaiomba Serikali kurekebisha sera yake ya elimu ili wasichana wenye umri mdogo wanaopata mimba wakiwa mashuleni kuendelee na masomo kwani kupata mimba si mwisho wa masomo.
Mkurugenzi huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 30 na bintiye akiwa na umri wa miaka 15 anasema mpaka sasa asasi yake imesadia wasichana zaidi ya 200 walioshindwa kuendelea na masomo mkoani hapa, kati yao mabinti wadogo 15 waliojifungua amewapeleka kusoma fani mbalimbali katika vyuo vya ufundi ikiwamo mapishi, cherehani, umeme na wengine wakipata ushauri juu ya ujasiliamali.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Haki Elimu, John Kalage naye akaeleza vikwazo vinavyowakabili watoto wa kike mashuleni kuwa ni pamoja na changamoto za kimazingira, kiutamaduni, kiuchumi na kimazoea ambazo zimekuwa zikirudisha nyuma haki ya upatikanaji wa elimu bora kwa mtoto wa kike nchini.
Kalage anasema elimu ya mtoto wa kike inahitaji tafakari na mawazo ya juu zaidi kutokana na kuwa na mahitaji maalumu ya ziada na hatari zinazowakabili watoto wa kike na kupelekea kukosekana usawa kati yao na watoto wa kiume katika kupata elimu.
“Kwa kutambua hili, suala la ulinzi wa mtoto hususani mtoto wa kike na wale wenye mahitaji maalumu ni suala ambalo Haki Elimu imelipa kipaumbele katika mpango mkakati wake mpya wa mwaka 2017/2020,” anasema Kalage.
Mkurugenzi huyo anatoa mfano mwaka 2015 kuwa jumla ya watoto wa kike 69,067 wa shule za msingi na sekondari waliacha shule kwa sababu mbalimbali zikiwemo mimba, utoro na vifo huku akiiomba Serikali kujitahidi kudhibiti sababu hizo.
Agizo la JPM
Julai 4 mwaka huu 2017, Rais John Magufuli akiwa wilayani Sengerema mkoani Mwanza katika uzinduzi wa mradi wa maji, alizungumzia kuhusu elimu bure na suala la wanafunzi wa kike kupata mimba wakiwa shuleni na alionya akiwataka wanafunzi kufuata elimu iliyowapeleka shuleni na si vinginevyo na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitakuwa tayari kulifurahia na kuwataka wazazi kusimama kwa nafasi zao.
Viongozi Halmashauri Kilombero
Kaimu Ofisa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Nicholaus Mkenda anakiri kuripotiwa taarifa ya mimba ya mwanafunzi huyo na kwamba bado kumekuwa na tatizo la wanafunzi wa kike kupewa mimba na watuhumiwa kukimbia.
Pia, Mkenda anasema kama wilaya bado kumekuwa na changamoto ya umbali ambao umekuwa ukisababisha wanafunzi kutembea kwa muda mrefu kufuata masomo na hiyo ni kutokana na jiografia ya wilaya hiyo, huku watoto wa kike wakikutana na vishawishi vinavyosababisha kupata mimba.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Dennis Londo anasema kwa sasa wamekuwa wakali zaidi na kuchukua hatua kwa wale wote wanaosababisha na kuwapa mimba kwa watoto wa shule.
Londo anasema halmashauri inachokifanya ni kuangalia namna gani bora ya kudhibiti na kufuata kanuni zilizopo, kwani kupata ujauzito ukiwa shuleni ni kosa hivyo wengi wao wamefikishwa katika vyombo vya sheria.

Sambaza kwenye Google Plus

Kuhusu mguta

Hii ni Blog yenye jukumu la kukupasha habari za Mtanzania mwenye hali ya chini ambaye hajapata nafasi ya kutoa maoni yake.

0 Michango:

Post a Comment