//
Ads

Wakulima wapewa dawa ya kuwazuia Tembo

Na Mwandishi Wetu
WAKULIMA wa kijiji cha Mtipule kata ya Msongozi, Mvomero mkoani Morogoro, wametakiwa kuendelea na shughuli zao kilimo kwani tatizo la Tembo waliokuwa wakiharibu mazao yao limepatiwa ufumbuzi.

Wakulima hao kutoka kaya 48 za kijiji hicho, waliotelekeza mashamba yao kwa miaka minne mfululizo kwa kuhofia Tembo kuharibu mazao yao, kurejea kulima kwa kufuata ushauri wa kitaalamu waliopewa kukabiliana na wanyama hao.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Luanda Kalunga amesema hayo jana kwenye kikao kilichoandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali inayoshughulika na masuala ya uhifadhi wa jamii (CONASU) wakati wakipewa elimu ya mradi wa kuimarisha ushiriki wa jamii kwa kutunza na kuhifadhi makazi ya Tembo katika hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwenye mradi uliofadhiliwa na mfuko wa misaada wa Uingereza ujulikanao kama The Rufford Foundation (RSG) na kufanyika kijijini hapo.

Kalunga amesema kuwa wakulima hao walilazimika kutelekeza mashamba yao tangu mwaka  2012-2015 kufuatia Tembo kula na kuharibu mazao yao kila msimu wa kilimo.

Amesema Tembo hao wamekuwa waharibifu hadi kufikia kujeruhi na kuua wakulima wanaowakuta mashambani ambapo mpaka sasa tayari wameshaua watu wawili na kumjeruhi mmoja.

Aliwataja waliouawa na Tembo kuwa ni pamoja na Josephat John na Emmanuel Valentino  ambapo aliyejeruhiwa ni mkulima aliyefahamika kwa jina moja la Kazulege ambaye hadi sasa anatumia mipira kupata haja ndogo.

Hivyo Mwenyekiti huyo aliwataka wakulima hao kuacha hofu na kurejea mashambani kwani tayari wameshapata na wanaendelea kupata elimu ya kukabiliana na Tembo kwa kuweka mizinga ya nyuki itakayomfanya Tembo kutopita shambani na kula au kufanya uharibifu wowote.

Hata hivyo Kalunga aliwataka wakulima hao kuhakikisha wanalima mazao kwenye mashamba yao msimu huu na hata kama hawalimi wasafishie kufuatia kuzidi kuwa msitu na kusababisha mashambapori yanayoweza kuwa maficho ya wanyama na kwamba atakayekiuka atafikishwa mahakamani.

“Kijiji hiki kipo jirani na hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Tembo wanaharibu mazao yetu na tunajazwa kwenye malipo ya fidia lakini kila mwaka hatulipwi, nadhani ndio pia imewafanya wakulima wasuse kulima,” amesema Kalunga.

Akizungumza kwenye kikao hicho Meneja wa Mradi huo, Angelus Runji amesema kuwa kufuatia kupata mradi huo wa miezi minane kwenye vijiji vitano vya wilaya za Mvomero na Kilosa watahakikisha wanaondoa dhana mbaya ya wakulima kumchukia Tembo badala ya kumtunza na kumlinda na kufanya agizo lililotolewa na Serikali kutekelezwa.

“Jamii ya vijiji hivi inaona uwepo wa Tembo ni sawa na janga au shida kubwa tofauti na malengo na matakwa ya Serikali juu ya uhifadhi na ulinzi wa Tembo kama Rasilimali ya Taifa,” amesema Runji.

Meneja huyo amewaasa wakulima wa kijiji hicho kuupokea na kuutekeleza mradi huo wa ufugaji nyuki kwa ajili ya kuzuia Tembo kupita au kusogea mashambani kufuatia Tembo kuwa adui wa nyuki na kufanya kuendeleza shughuli zao za kilimo na kuzifanya kuwa na tija kwao.
Sambaza kwenye Google Plus

Kuhusu Anonymous

Hii ni Blog yenye jukumu la kukupasha habari za Mtanzania mwenye hali ya chini ambaye hajapata nafasi ya kutoa maoni yake.

0 Michango:

Post a Comment