Mchungaji, Josephat Gwajima akiwasili kituo kikuuu cha Poisi (Central) |
Na mwandishi wetu
NI kama shughuli
zilisimama kwa saa kadhaa katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam
wakati watu wawili maarufu nchini, Askofu Josephat Gwajima na mfanyabiashara
Yusuf Manji waliporipoti kituoni hapo wakitaka wahojiwe.
Wawili hao, pamoja na
wengine 63 walitakiwa waripoti kituoni hapo leo kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu
biashara ya dawa za kulevya, utumiaji au kama wana taarifa zinazoweza kusaidia
Jeshi la Polisi kukomesha biashara hiyo haramu.
Wito huo ulitolewa na
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye juzi aliita waandishi
ofisini kwake na kutaja orodha ya watu 65, wakiwemo wanasiasa, wafanyabiashara
na viongozi wa dini.
Lakini, Manji, ambaye ni
mwenyekiti wa moja ya klabu kubwa nchini ya Yanga, na Askofu Gwajima,
anayeongoza kanisa la Ufufuo na Uzima, walienda kituoni hapo jana na
walisikindikizwa na mashabiki na waumini wao.
Manji, ambaye ni
Mwenyekiti wa Kampuni ya Quality Group, alifika kituoni hapo saa 4:54 asubuhi
akiwa wa kwanza na alifika akiwa ndani ya gari aina ya Range Rover ya rangi
nyeusi, akifuatana na watu wawili alioingia nao kituoni.
Dakika chache baada ya
kuingia, Manji alitoka ndani na akawa anazungumza na watu waliovalia sare na
wengine kiraia na baada ya muda aliingia tena ndani ya kituo.
Ilipotimu saa 6:10
mchana, Manji alitoka na kuonekana anaondoka, lakini alipofika getini askari
walimfuata na wakarudi naye ndani.
“Mzuie, mzuie, mzuie,”
alisikika mmoja wa polisi akisema wakati Manji akionekana kuondoka.
Mfanyabiashara huyo alitii amri na kurudi kituoni.
Wakati Manji akiwa ndani
ya kituo hicho, saa 7:33 mchana Askofu Gwajima aliwasili akiambatana na watu
wapatao 10 walioonekana kuwa ni viongozi wa kanisa hilo na wote wakaingia
kituoni.
Wakati viongozi hao
wakiwa ndani, saa 8:00 mchana waumini takribani 20 walionekana kuwa ni wa
kanisa la Ufufuko na Uzima walifika wakiwa wamevalia suti nyeusi.
Waumini hao wa kike na
kiume walikusanyika nje ya kituo hicho na kujipanga mstari nje ya geti la
kuingilia kituoni, lakini askari waliwazuia na kuwataka kukaa mbali na eneo
hilo ili wasubiri hatma ya askofu wao.
Taarifa kutoka ndani ya
kituo hicho zilisema kuwa watuhumiwa hao hawakutoa maelezo yoyote kwa sababu
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro alikuwa kwenye kikao
ofisini kwa Makonda.
Eneo hilo pia lilifurika
mashabiki kadhaa wa klabu ya Yanga waliokuwa wakifuatilia hatma ya Manji.
Baada ya ukimya
uliotawala eneo hilo huku waandishi wa habari wakifuatilia matukio hayo kwa
mbali kutoka nje, Manji na Gwajima walionekana wakitoka kituoni saa 10:27 jioni
na wote kupanda gari dogo jeupe aina ya Toyota Land Cruiser na kuondoka.
Baada ya kurejea,
Kamanda Siro aliwaambia waandishi wa habari kuwa hangeweza kuzungumzia suala
hilo jana.
Gwajima amvaa Makonda
Awali, Gwajima
alizungumza na waumini wa kanisa lake na kumuomba Rais John Magufuli
ambadilishe kazi Makonda, akimsifu kuwa ni mchapakazi, lakini hawezi kazi ya
utawala kutokana na ama kutokomaa au kutokuwa na uzoefu.
Akijibu maswali ya
waandishi wa habari baada ya kuongea na waumini, Askofu Gwajima alisema kitendo
cha Makonda kumtaja hadharani akihusishwa na dawa za kulevya kinaonyesha ana
nia ovu na kanisa hilo.
“Sisemi Magufuli
amfukuze kazi, hapana, Makonda ni jasiri na mchapakazi, lakini kazi ya utawala,
kuongoza watu imemshinda atamharibia Rais,” alisema.
“Usalama wa Taifa
watakuwa wanafahamu kama Askofu Gwajima anahusika au hahusiki kwa namna moja
ama nyingine na dawa za kulevya. Kitendo cha Makonda kunitaja kupitia vyombo
vya habari kinaonyesha ana chuki na mimi na hajui masuala ya utawala.
“Hivi hafahamu kwamba
nina waumini zaidi ya 70,000, nina makanisa 400 na maaskofu 25. Ameshindwa vipi
kuchunguza na kuniita hadi atangaze kwenye vyombo vya habari?”
Alisema sababu nyingine
ya kutaka Rais Magufuli ambadilishe kazi ni kutokana na viongozi wa Serikali
hivi sasa kufanya kazi kwa hofu.
“Mawaziri, wakuu wa
mikoa wanaogopa wanaposikia sauti ya Makonda, wanadhani kila anachofanya
ametumwa na Rais Magufuli. Si kweli anawatisha tu huyo,” alisema.
“Magufuli amekuwa
akimpongeza Makonda kwa kazi nzuri anazozifanya, lakini si kila anachofanya
anatumwa na Rais.”
Aliwataka viongozi
wengine kutokuwa na hofu na Makonda kwa kuwa anachokifanya ni kuwatisha wenzake
kwa kutumia jina la Rais.
“Nimekuwa nikijiuliza
sifahamu chochote kuhusu dawa za kulevya, huyu Makonda ananipakazia hivi ili
kumfurahisha nani?” alihoji.
Wivu na chuki binafsi
Askofu Gwajima alisema
hivi karibuni walikuwa kwenye mechi ya soka kati ya viongozi wa dini na wa
serikali ambayo yeye na Makonda walicheza timu moja.
“Kwa kuwa nilichelewa,
niliamua kutumia helikopta hadi uwanjani lakini wakati tukicheza mpira, Makonda
alikuwa ananiangalia kwa jicho la chuki mpaka nikawa nashangaa. Sasa leo
nimeamini kijana mwenzangu ana chuki binafsi,” alisema.
Alisema Makonda
anatakiwa kufahamu kwamba si kila anayefanikiwa kiuchumi anakuwa anajihusisha
na dawa za kulevya.
Askofu Gwajima alisema
ana shahada ya uzamivu ya filosofia (PhD) na hulipwa dola 1,000 za Kimarekani
(sawa na zaidi ya Sh2.2 milioni) kwa saa anapofanya uhadhiri vyuoni.
“Nimetoka Japan ambako
nilikaa miezi mitatu, unadhani nitachuma kiasi gani?” alihoji.
“Sasa kijana mwenzangu
Makonda asiwe na chuki binafsi, bali angeniuliza unapataje fedha, lakini si
kuvunja heshima yangu niliyoijenga siku nyingi.”
Alisema hajawahi kunywa
pombe, kuvuta sigara na wala hajui dawa za kulevya zikoje.
Makonda kanisani
Gwajima alisema Makonda
akiwa na spika wa zamani wa Bunge, Marehemu Samuel Sitta waliwahi kufika
kanisani kwake kuombewa.
“Nilimkaribisha Makonda
madhabahuni na akazungumza na waumini akisema ni heshima kubwa kupata nafasi
ile na tulisali pamoja. Je, kipindi kile hakuhofia kuwa nahusika na dawa za
kulevya?” alihoji.
Nisirudishwe kwa Lowassa
Alipoulizwa kama
patashika anazopata zinatokana na kuwa karibu na aliyekuwa mgombea wa Chadema,
Edward Lowassa, mchungaji huyo alisema anashangaa kuona anarudishwa kwa mtu
aliyeona anafaa kuwa Rais.
“Wakati wa uchaguzi kila
mtu aliona mtu aliyefaa kuwa Rais na mimi niliona Lowassa ndiye aliyekuwa
anafaa kuwa Rais,” alisema Gwajima.
“Lakini bahati nzuri
Lowassa hakuchaguliwa na badala yake amechaguliwa Magufuli ambaye anafanya kazi
ambayo ingeweza kufanywa na wapinzani. Kwa hiyo namuunga mkono. Nashangaa
kwamba mimi namuunga mkono, lakini wanazidi kunirudisha kwa yule.
“Mimi si mnafiki. Wakati
Rais Jakaya Kikwete akiwa madarakani niliikosoa sana Serikali yake, lakini
nashukuru sasa Magufuli anafanya kazi zilizotarajiwa na Watanzania wengi, ndiyo
maana mara nyingi nampongeza.”
0 Michango:
Post a Comment