Na Mwandishi Wetu
WAKAZI 778 wakijiji cha Mtipule kata ya Msongozi, Mvomero mkoani Morogoro wapo hatarini kukumbwa na magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindupindu kufuatia kutokuwa na huduma ya maji safi na salama kwa miaka 10.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Luanda Kalunga amesema wakazi hao wamekosa huduma hiyo ya maji safi na salama kwa muda mrefu sasa tangu mwaka 2002 kufuatia visima vyao vya malingi viwili kukauka maji, hivyo kulazimika kutumia maji ya kwenye madimbwi ya mvua.
Amesema wanalazimika kutumia maji hayo ambayo si salama kutokana na wakazi hao kushindwa kumudu gharama za kununua maji safi ambayo yanauzwa kati ya Sh. 500 na 700 kwa dumu moja la lita 20 jambo linalowapa wakati mgumu wanakijiji kununua kutokana na hali mbaya ya uchumi waliyonayo.
Hivyo Kalunga aliiomba Serikali, Halmashauri na Mbunge wa jimbo hilo, Suleiman Sadiq kuwatazama kwa jicho la huruma kwa kutambua na kutatua changamoto hiyo ya maji inayowakabili kwani ni hatari kwa mlipuko wa magonjwa hasa katika kipindi cha mvua.
Wakizungumzia hilo, Beatrice Nestor aliyekutwa akichota maji ya mvua yaliyotuama kwenye dimbwi, amesema kuwa shida ya maji katika kijiji hicho huwafanya wakati mwingine kushindwa kuoga hata wiki hadi mwezi ambapo msimu wa mvua ukianza hutumia maji hayo kwa kufulia, kuoga na wengine hutumia hata kwa kunywa na kupikia.
“Mvua ikinyesha hivi kwetu ni neema, utakuta watu tunaoga kwenye mvua na wengine tukichota maji ya madimwi kwa ajili ya kufulia na kuoga nyumbani na wengine hutumia kunywa na hatakupikia chakula, tunaumwa matumbo mara kwa mara,” amesema.
Naye Anna Saidi alimuomba Mbunge wa jimbo hilo kukumbuka ahadi yake ya maji aliyowapa wakati akifanya kampeni ya uchaguzi 2015 katika kijiji hicho kwa kuweka angalau bomba moja la maji safi ambapo alidai anaweza kuwaokoa na magonjwa mbalimbali ya matumbo na ngozi.
Naye Mbunge wa jimbo la Mvomero, Suleiman Sadiq aliwataka wakazi hao kuwa na subira na ahadi walizopewa kwani ahadi hutekelezwa ndani ya miaka mitano ya uongozi ambapo kwa sasa wapo kwenye mipango mizuri huku wakisubiri mafungu yaliyotengwa kwenye bajeti ndipo waanze kutekeleza ahadi za wananchi.
0 Michango:
Post a Comment