Na Mwandishi wetu
TAARIFA KWA UMMA
SERIKALI YAELEZA
UTEKELEZAJI WA MASUALA MBALIMBALI BUNGENI
Dodoma, Jumanne,
Januari 31, 2017:
SERIKALI leo
imeainisha utekelezaji na kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya maendeleo
kwa wananchi katika sekta mbalimbali katika kikao cha kwanza cha Mkutano wa
Sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Majibu ya Serikali kwa baadhi
ya hoja ni kama ifuatavyo:
Ujenzi Nyumba za Walimu
Akijibu hoja kuhusu
ujenzi wa nyumba za walimu, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, ameliambia Bunge kuwa Serikali ilitenga kiasi
cha Sh. Bilioni 13.9 katika Bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba
za walimu wa Sekondari, na Shilingi bilioni 11.4 kwa nyumba za walimu wa Shule
za Msingi.
Aidha, Waziri Jafo
ameeleza kuwa tayari nyumba 146 za walimu zimeshajengwanc hini kupitia Mpango
wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari. Pia amezungumzia Serikali kuanza kulipa
madeni ya walimu.
Ujenzi wa Viwanda Nchini.
Akijibu swali kuhusu
uwekezaji wa viwanda nchini hususani mkoani Tabora ambako kuna kilimo cha
Tumbaku na maeneo mengine yenye malighafi, Mhandisi Edwin Ngonyani kwa niaba ya
Waziri wa Viwanda ameliambia Bunge kuwa tayari Serikali imeshafanya mazungumzo
na wawekezaji kutoka Vietnam na kuzitaka Halmashauri zote nchini kuendelea
kuitikia wito wa kutenga maeneo ya uwekezaji.
“Kituo cha uwekezaji
Nchini (TIC) kimepewa maelekezo maalum kunadi fursa hii
kwa wawekezaji katika
sekta ya tumbaku na sigara hapa nchini,” alisema Mhandisi Ngonyani ambaye pia
ni Naibu Waziri, Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Tupende Bidhaa Zetu
Akijibu hoja kuhusu
bidhaa nyingi za Kenya kuingia nchini, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Suzan Kolimba amesema moja ya changamoto
inazozikumba bidhaa za Tanzania ni wananchi wake kupenda vya nje.
“Katika kukabiliana na
changamoto hiyo, Serikali iliunda Kamati ya Kitaifa ya Kudhibiti na Kusimamia
Uondoaji wa wa Vikwazo visivyo vya Kiforodha na kuhamasisha wafanyabiashara
nchini kuzalisha bidhaa zenye ubora,” alisema.
Serikali yagharamia 100% umeme vijijini.
Serikali imesisitiza
kuwa inagharamia ujenzi wa umeme vijijini kupitia Wakala wa Kusambaza Umeme
Vijijini (REA) kwa asilimia 100. Akijibu maswali ya wabunge, Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, alisema wananchi wanalazimika
kuchangia Sh. 27,000 tu ambazo ni gharama za kodi ili waunganishiwe huduma hiyo
wakati mradi ukiwa unaendelea.
“Lengo ni kuhamasisha
na kuwawezesha wananchi wa vijijini wenye vipato vidogo kuweza kupata huduma za
umeme kwa gharama nafuu,” alisema akisisitiza kuwa wale ambao huomba huduma
hiyo baada ya wataalam wa REA kumaliza kazi yao ndio hulazimika kulipia umeme
huo kwa Sh. 177,000 tu badala ya Sh. 320,960/wanazotozwa wakazi wa mijini kwa
umbali usiohitaji nguzo.
Bei ya maji kupungua.
Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge amesema Serikali itaendelea kupunguza
gharama za maji nchini hasa vijijini kadiri gharama za umeme zitakavyoendelea
kupungua hasa wakati huu nchi inapoingia katika uchumi wa gesi.
Aliongeza kuwa kwa
upande wa vijijini miradi ya umeme wa jua na nishati nyingine za bei nafuu pia
itasaidia kupunguza gharama za umeme na kusaidia wananchi kupata maji katika
miradi mingi inayondelea sasa nchini.
Madai ya Unyanyasaji Zanzibar
Serikali imewataka
wananchi wote wanaodai kufanyiwa unyanyasaji na vikosi vya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kutoa taarifa za matukio hayo polisi ili hatua stahiki
zichukuliwe.
Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema kwa kuwa hakuna tarifa za kuripotiwa kwa
matukio hayo katika kituo chochote cha Polisi, atachukua pia hatua za kutuma
maafisa wake kufanya uchunguzi zaidi.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi Idara ya
Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.
0 Michango:
Post a Comment