Na Mwandishi wetu
MWENYEKITI wa kikao
cha jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, kinachoendelea Arusha, Bernard
Luanda, leo amegeuka mbogo kwa wanasheria wa serikali kwa kitendo cha kumnyima
Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema dhamana kwa lengo la kumnyima haki.
Akizungumza Mahakamani
hapo leo mbele ya majaji wenzake Stella Mugasha na Jaji Kipenka Mussa, Luanda
amesema haipendezi na haingii akilini mtu (Lema) kushikiliwa kwa miezi minne
bila sababu kwa misingi ya kumnyima haki.
“Tunaomba ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa serikai (DPP) muwe makini sana maana mnatufanya wanasheria
wote hatuna akili na mnachafua Mahakama, kwa hali ya kawaida mtu mumshikilie
kwa misingi ya kisheria, lakini katika kesi hii tumepitia jalada hatujaona kitu
chochote cha kumshikilia Lema hadi leo na imetushitua sana,” alisema huku
akishauriana na wenzake mara kwa mara kwa masikitiko.
Aliendelea kusema kuwa
ofisi ya DPP inaitia najisi taaluma hiyo, kitu kipo wazi ila wanafanya vitu vya
ajabu na havipendezi.
Alihoji jaji Luanda
kuwa “Tumesoma faili lote tunashangaa hivi kweli ofisi ya mwanasheria mkuu ina
wanasheria kweli na kama wapo kwa nini huyu mtu (Lema) awe ndani mpaka leo?”.
Alisema kwa kuwa
mikono yao kisheria imefungwa hawawezi kufanya chochote kwa leo na kuwataka
Mawakili upande wa Lema kurudi Mahakama Kuu, kuendelea na maamuzi ya dhamana.
Hali hiyo ilitokana na
Wakili wa serikali Faraja Nchimbi kusimama mahakamani hapo na kuomba kuiondoa
rufaa hiyo kwa madai kuwa ipo nje ya uwezo wake.
“Waheshimiwa Majaji
baada ya timu yetu ya wanasheria kupitia kwa kina rufaa hii kwa sababu
zisizozuilika tumeona hatupo tayari kuendelea na rufaa hii, maana hatukupeleka
kusudio (Notisi) kwa msajili muda ulipita, hivyo tunaomba kuiondoa na uamuzi wa
kuiondoa rufaa hii tumeufikia Ijumaa muda uliisha kuja mahakamani,”. Alisema
Nchimbi.
Baada ya kuwasilisha
ombi hilo, Wakili wa Lema Peter Kibatala, alisimama na kusema upande wao hawana
pingamizi ila waliomba hoja za awali za rufaa hiyo ziondolewe Mahakamani hapo
bila kunakiliwa.
Baada ya ombi hilo
Jaji Kipenka Mussa alipokea kwa niaba ya Majaji wenzake na kukubali ombi la
kuiondoa rufaa hiyo namba 9/2017.
Aidha Jaji Luanda
alimkaribisha jaji Stella Mugasha pia kuongea kwa niaba yao ambapo alisema
mahakama imekubali ombi la pili la kuiondoa rufaa namba 10/2017, baada ya
Wakili Paul Kadushi kuomba kuiondoa pia.
Wakili wa Lema Peter
Kibatala, alilazimika kusimama tena Mahakamani hapo kusema kuwa upande wao
unasikitika kuona ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na DPP wanatumia
Mahakama kwa njia ya kumnyima haki mteja wao, hivyo aliomba mahakama hiyo
iwatatulie tatizo la kisheria lililojitokeza hadi mteja wao awe ndani hadi
sasa.
Kibatala aliongea hayo
huku akishindwa kujizuia na kumwaga chozi la huzuni mahakamani hapo mbele ya
Majaji hao.
0 Michango:
Post a Comment