![]() |
Edward Lowassa |
Na Mwandishi wetu.
EDWARD Lowassa,
aliyekuwa mgombea urais kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
mwaka 2015 ameungana na viongozi wa dini na wanasiasa nchini katika kile
kinachoonekana kuwepo kwa mwelekeo mbaya wa upatikanaji wa chakula nchini na
kutaka tahadhari ichukuliwe.
Hayo yanafanyika huku Rais
John Magufuli akigoma kutambua hali hiyo ya upungufu wa chakula na baa la njaa
kwa baadhi ya maeneo nchini.
Pia Taasisi ya Baraza
Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC)
zimewataka waumini wao kuomba mvua kutokana na baa la nja nchini.
“Serikali imesema
haitoi chakula, mimi nimejadiliana na chama changu tumeona tufanye mpango wa
kuwatafutia chakula Watanzania.
“Hata kama ni kutoka
nje ya nchi ninaamini dunia itatusiia,” ameeleza Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu
kwenye mkutano wa kampeni za Udiwani Bukoba.
Kauli
ya Lowassa na viongozi wa dini inakwenda kinyume na ile aliyoitoa Rais John
Magufuli alipokuwa mjini Bariadi mkoani Simiyu ambapo alisema, suala la kuwepo
kwa njaa ni uzushi na kwamba, yeye ndiye mwenye mamlaka ya kutoa taarifa za
njaa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Kwenye
mkutano huo Rais Magufuli alidai taarifa za kuwepo kwa njaa zinasababishwa na
wafanyabiashara ambao wamezoea pale panapokuwepo na ukame wanatumia vyombo vya
habari kudai kuwepo njaa.
“Wapo
wafanyabiashara wengine wachache waliokuwa wamezoea panapotokea matatizo kidogo
tu ya ukame wanatumia vyombo vya habari ikiwa pamoja na magazeti wanayoyaamini
wao sio magazeti yote, pamoja na baadhi ya wanasiasa kuzungumza Tanzania kuna
njaa.
“Anayejua
njaa ni Rais na sio gazeti fulani mimi ndiyo niliyepewa dhamana ya kuwaongoza
Watanzania,” alisema.
Pamoja na kauli hiyo
taasisi kubwa zinaeleza kuwepo kwa baa la njaa kwa baadhi ya maeneo ikiwa ni
pamoja na upungufu wa chakula nchini kutokana na kuwepo kwa ukame.
Tayari viongozi wa
siasa wameeleza kuwepo kwa njaa na kuitaka serikali kuchukua hatua badala ya
kuamini kinyume na hali halisi akiwemo Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha
ACT-Wazalendo.
“Kama Watanzania
watakufa njaa kutokana na kutochukuliwa hatua sasa, serikali itakuwa kwenye
wakati mgumu,” amesema Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini huku akiitaka serikali
kutekeleza wajibu wake kwa wananchi.
Zitto ametoa tahadhari
hiyo alipokuwa kwenye mkutano wa kampeni za udiwani Kijichi jijini Dar es
Salaam na kwamba, wanasiasa wanatumia wasaa wa mikutano ya kisiasa
iliyoruhusiwa kwa sasa kueleza hali halisi ya nchi.
Lowassa amemtia
majaribuni Rais Magufuli kwa kumtaka kutafakari upya kauli yake kuhusu hali ya
chakula nchini.
“Mashirika makubwa ya
dini nchini yamethibitisha kuwa kuna uhaba wa chakula lakini serikali bado
inaendelea kukana tatizo hilo. Narudia namuomba rais atafakari upya kauli zake
kuhusu suala hili,” amesema Lowassa.
0 Michango:
Post a Comment