//
Ads

Rais Magufuli awavua nguo wasaidizi wake


Na Hamisi Mguta

KUFUATIA kauli ya Rais John Magufuli kuwaruhusu wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga wa jijini Mwanza, na kusababisha wafanyabiashara hao nchi nzima kurudi katika maeneo waliyohamishwa, mchambuzi wa mambo ya siasa Dotto Bulendu amechambua hatua hiyo.

Bulendu ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Kijamii wa Facebook, msome hapa chini:-  

Nikiwa mwanafunzi Chuo Kikuu Mzumbe, nilisoma somo linaitwa utawala bora (Good governance), niliambiwa dhana hii ya utawala bora ina misingi yake, miongoni mwake ni Rule of law (utawala wa sheria), matumizi sahihi na stahiki ya rasilimali, haki za binadamu, ushirikishwaji, uwajibikaji n.k.

Dhana ya uwajibikaji niliambiwa imegawanyika katika mafungu matatu, uwajibikaji wa kisheria (legal accountability), uwajibikaji wa kiutawala (administrative accountability) na uwajihikaji wa kisiasa (political accountability).

Dhana zote hizi tatu zinagawanywa katika makundi mawili, uwajibikaji wa pamoja (collective accountability) na uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja (individual accountability).

Wataalam wa masuala ya uongozi wanasema katika maeneo yote matatu ya uwajibikaji, kitaasisi ama kiserikali kila mnapowajibika inashauriwa kuzingatia dhana ya uwajibikaji wa pamoja (collective accountability) ,dhana hii inasaidia kuonesha mnaowaongoza kuwa mpo pamoja, mnafanya mambo pamoja, individual accountability ina ukakasi kutokana na kuweka uwezekano wa kuonesha kuwa kila mtu ana lake.

Kilichofanyika kwenye sakata la Machinga jijini Mwanza, ni kuonesha kuwa serikali haizingatii misingi ya utawala bora hususuni uwajibikaji wa pamoja (collective accountability).

Kitendo cha Rais kusubiri wasaidizi wake wawafurushe machinga na yeye aje kuwarudisha huku akitumia lugha ya kuwatisha, kitaalam inaitwa "individual accountability" huu ni mfumo ambao kila mtu anawajibika kivyake, tatizo la mfumo huu mlio chini kila siku mtaonekana hamfai, mkuu anakuwa katika nafasi kubwa ya kujisafisha ili aonekane hana kosa, mlio chini mnabidi muwe makini kwenye kuamua jambo lolote.

Athari za individual accountability inaweza onesha kama taasisi ama idara hampo pamoja, hamna dira wala maono, kila mtu anafanya atakavyo.

Si mfumo mzuri kiutawala,huu mfumo wa uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja ndiyo alioutumia Rais kutatua tatizo la machinga, Rais kawavua nguo wasaidizi wake, sijui wasaidizi wa Rais jijini mwanza wanazificha wapi sura zao?

Kama Rais angekuwa anaongoza kwa kuzingatia msingi wa uwajibikaji wa pamoja, katazo hili angelifanya kabla ya siku ya utekelezwaji wa zoezi hilo na katazo hilo asingelitoa yeye,angemwambia mkuu wa mkoa asitishe na Tangazo hilo lingetolewa na mkuu wa mkoa ili wawe na heshima mbele ya jamii ya watu wanaowaongoza.

Mfumo alioutumia Rais umewavua nguo wasaidizi wake, kawapora nguvu zote walizokuwa nazo, sasa si lolote mbele ya jamii ya machinga.

Nadhani Rais angebalidi style yake ya kuongoza asiongoze kwa dhana ya uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja, atumie dhana ya uwajibikaji wa pamoja (collective accountability), madhara ya individual accountability, inajenga hofu kwa wasaidizi, inaweza sababisha wasaidizi wako wakawa waoga kutenda jambo wakihofia kudhalilika kama ilivyowakuta viongozi mkoani Mwanza.

Kama Rais ana nia njema na viongozi wa mkoa wa Mwanza, ni vizuri akawapa uhamisho viongozi hawa, kiutawala Mh Rais ni vizuri akabadilisha style yake.
Sambaza kwenye Google Plus

Kuhusu Anonymous

Hii ni Blog yenye jukumu la kukupasha habari za Mtanzania mwenye hali ya chini ambaye hajapata nafasi ya kutoa maoni yake.

0 Michango:

Post a Comment