//
Ads

Wanafunzi Mzumbe watwisha zigo la Tanzania ya Viwanda


SERIKALI imekitaka Chuo Kikuu Mzumbe na vyuo vikuu vingine nchini kuongeza juhudi katika utafiti na ubunifu kufuatia mawazo na kazi zao kuweza kutumika sambamba na kupata wataalamu zaidi ili kuendeleza azma yake ya kujenga Tanzania ya viwanda.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doroth Mwanyika kwa niaba ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji wakati wa kongamano la kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere lililohusisha wanafunzi, wahadhiri na wanazuoni.

Mwanyika alisema kuwa kufuatia Mwalimu Nyerere alikuwa muumini mkubwa wa nafasi ya ubunifu katika maendeleo ikiwa ni pamoja na viwanda hivyo Mzumbe hawana budi wanapoendelea kuazimisha kumbukumbu yake kufikiri zaidi namna ya kukuza ubunifu na vipaji miongoni mwa wataalamu na wanafunzi kama njia ya kumuenzi Mwalimu.

Alisema, ikiwa vyuo vikuu vitaongeza juhudi katika masuala ya utafiti na ubunifu utavifanya viwanda kuzalisha bidhaa bora na zinazokidhi viwango vya soko la ndani na nje ya nchi.

“Chuo kikuu Mzumbe kinafundisha na kuzalisha wataalamu katika fani za uchumi, biashara, masoko, fedha na uhasibu, TEHAMA, Ujasiriamali, uongozi na Menejimenti, sheria na zinginezo, kina nafasi kubwa sana katika kuleta mawazo mapya na ya kimapinduzi katika sekta ya viwanda,” alisema Mwanyika.

Profesa Peter Kuzirwa alisema, ipo haja ya kuwa waangalifu sababu inapoingizwa suala la viwanda kwani nchi nyingi tayari zimeshapiga hatua jambo ambalo litasababisha kuwepo na ushindani wa hali ya juu.

Profesa Kuzirwa alisema, upo umuhimu wa kulinda viwanda vitakavyoanzishwa na vilivyopo sambamba na kuwa washindani wa masoko mbalimbali yakiwemo ya Nchi za China na Korea.

Naye Profesa Josephat Itika alishauri Serikali inapotaka kuwekeza kwenye viwanda iweke vipaumbele madhubuti vitakavyozuia nchi kurudia makosa yaliyotokea kwa viongozi waliopita ambao nao walikuwa na nia ya kufanya nchi kuwa ya viwanda.

Alisema, lazima uwepo uongozi imara, kuwepo na nguvu kazi inayojituma kwenye sekta zote sambamba na kufanya jitihada kwa viongozi kuwa na nia thabiti ya kubadilika na kukubalina na mpango huo.
Sambaza kwenye Google Plus

Kuhusu Anonymous

Hii ni Blog yenye jukumu la kukupasha habari za Mtanzania mwenye hali ya chini ambaye hajapata nafasi ya kutoa maoni yake.

0 Michango:

Post a Comment