Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Chama cha ACT Wazalendo Mohamed Babu amesema chama chao kinafuatilia na kwa umakini mkubwa kuhakikisha usalama wa Kiongozi Mkuu wa chama chao Zitto Kabwe aliyekuwa amekamatwa jana usiku uwanja wa ndege.
Mwenyekiti huyo wa kamati ya ulinzi amewataka wanachi na wanachama wa ACT wazalendo kuwa watulivu katika kipindi hichi ambacho kiongozi wao yupo chini ya ulinzi kwani Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Chama inafuatilia hatua kwa hatua kwa umakini kuhakikisha Usalama wa Zitto Kabwe
Aidha katika taarifa aliyoitoa kwenye ukurasa wao wa Chama cha ACT ameandika kwamba "Kiongozi wa Chama Ndugu Zitto Kabwe amesafirishwa na polisi usiku huu (saa kumi) kutoka kituo cha polisi cha Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es salaam kwenda Dodoma".
Jana Septemba 20, 2017 kulikuwa na taarifa kuwa Katibu wa Bunge Dkt. Thomas kashililah alitoa amri kwa jeshi la polisi kumkamata Mbunge huyo wa Kigoma Mjini na kutakiwa kumfikisha mjini Dodoma kwa ajili ya kuhojiwa katika Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge kutokana na kauli ambazo amewahi kuzitoa juu ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Job Ndugai pamoja na Bunge lenyewe kupitia mitandao ya kijamii.
Mhe. Zitto Kabwe alikamatwa na jeshi la polisi usiku wa jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam akitokea mkoani Kigoma.
0 Michango:
Post a Comment