Na Mwande Mtetezi
IKIWA unatawadha kwa kutumia chombo kama vile birika basi ni vema kama inawezekana liwe upande wako wa kulia na kama unatumia bomba basi fungua bomba lako kisha,
KWANZA : Anza kukosha vitanga vya
mikono yako huku ukisema ‘Bismillahir-rahmanir-rahiym.
Osha vitanga mara tatu.
PILI: Baada ya kuosha vitanga, tia
maji mdomoni na kusukutua mara tatu.
TATU: Halafu unapandisha maji
puani, kusafisha tundu za pua mara tatu.
NNE: Kisha ndipo uoshe uso wako
ukianzia na maoteo/mameleo ya nywele za kichwa mpaka mwisho wa kidevu kwa urefu
na toka ndewe moja ya sikio hadi nyingine kwa upana.Kuosha uso huambatana na
kutia nia moyoni kuwa sasa unatawadha na si vibaya kama ukitamka nia kwa ulimi
kama vile mtu kusema ‘Nawaytu ra-al Hadath au Nawaytu fardhal-wudhu’
au maneno yenye
kufanana na hayo. Vile vile uso huoshwa mara tatu.
TANO: Baada ya kukosha uso, sasa
ndipo uanze kuosha mikono ukianzia na mkono wa kulia.Ukoshe mkono huo tangu juu
ya kifupa panya mpaka vidoleni au kinyume chake na utafanya hivyo hivyo kwa
mkono wa kushoto. Ikumbukwe kuwa mikono nayo huoshwa mara tatu.
SITA: Kisha tena ndipo upake maji
sehemu ya kichwa mara tatu.
SABA: Kisha osha masikio yako,
ndani na nje mara tatu.
NANE: Halafu ndio umailizie
kutawadha kwa kuosha miguu yako, huku ukianzia na mguu wa kulia toka kifundoni
mwa mguu mpaka nyayoni, na utafanya hivyo hivyo kwa mguu wa kushoto ambao nao
utaosha mara tatu. Kwa utaratibu huu udhu wako utakuwa umekamilika na hivyo
kumaanisha kuwa sasa unayo rukhsa ya kusimama na kuzungumza na Mola wako ndani
ya swala.Utaratibu/mpango huu wa udhu unatokana na riwaya iliyopokelewa kutoka
kwa Imaam Ally -Allah amuwie Radhi - kwamba yeye alitawadha na (akaanza) kuosha
vitanga vyake mpaka akavitakasa, kisha akasukutua mara tatu na akauosha uso
wake mara tatu na (akaosha) mikono yake mara tatu na akapaka maji kichwa chake
mara moja kisha (ndipo) akaosha miguu yake mpaka vifundoni, kisha akasema :"Nilipendelea kukuonyesheni jinsi
ilivyokuwa twahara (udhu) wa Mtume wa Allah - Rehema na Amani zimshukie -" At-Tirmidhi.Hadithi
inayofanana na hii tuliyoitaja hapa imetajwa pia na Imaam Bukhariy katika
SAHIHI yake {kitabu cha hadithi} akiipokea kutoka kwa Sayyidna Uthmaan- Allah
amuwie Radhi-.
0 Michango:
Post a Comment