Kituo cha afya Mgeta, wilaya ya Mvomero, Morogoro
Na Mwandishi Wetu
WAKAZI wa Kijiji cha Lukuyu, Kata Mgeta, Mvomero wanaiomba Serikali kuwasadia kuanzisha ujenzi wa kituo cha afya ili kuwafanya kuepukana na adha ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa sita kusaka huduma ya afya.
Wananchi wa kijiji hiyo wanalazimika kufuata huduma ya afya katika kituo cha afya cha Mgeta huku akina mama wajawazito wakihatarisha maisha yao na watoto waliotumboni kwa kusafiri na pikipiki kwenda kujifungua.
Hayo yalibainishwa jana na Diwani wa Kata ya Mgeta Wilayani Mvomero, Godfrey Luanda wakati akifanya mahojiano maalumu mwandishi wa habari hizi mjini Morogoro.
Aidha alisema kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo kwani kwa sasa wameshaandaa mawe na matofali tayari kwa kuanza rasmi ujenzi wa kituo cha afya ifikapo mwezi Februari mwaka huu.
“Tunaiomba serikali na wadau kutusaidia ili kuweza kuanza rasmi ujenzi huo kwani tayari wananchi wamechangia nguvu kazi zao,’’alisema Diwani Luanda.
Hata hivyo alisema kukosekana kwa kituo cha afya katika kijiji hicho kunasababisha wakinamama wajawazito kuhatarisha maisha yao na watoto wanaowazaa kufuatia kutumia usafiri wa pikipiki kuwahishwa hospitalini huko.
Hivyo Diwani huyo alisema kuwa kijiji cha Lukuyu kina jumla ya wakazi 2,000 na hivyo kuiomba serikali na Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kuwaangalia wakazi hao kwa jicho la pili ili kuona ni jinsi gani ya kusaidia ujenzi huo ili kuweza kukamilika kwa wakati.
0 Michango:
Post a Comment