Virusi vya Zika vinaaminika kusababisha watoto kuzaliwa na vichwa vidogo
Na Mwandishi Wetu
Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu, NIMR imethibitisha kugunduliwa kwa virusi vya Zika nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dkt Mwele Malecela, virusi hivyo vimepatikana mkoani Morogoro, Mashariki mwa Tanzania na mkoani Geita, kaskazini magharibi mwa Tanzania.
Utafiti huo ulifanyika kutokana na uhalisia kuwa kuna mazingira yanayowezesha kuzaliana kwa mbu wanaoeneza virusi hivyo.
Dk. Mwele Malecela amesema kwa sasa serikali inaangazia kuzuia wajawazito wasiumwe na mbu ambao wanaaminika kueneza virusi hivyo.
"Bado tunajaribu kuangalia ni aina gani ya virusi vya Zika. Lakini hiyo ni dhahiri, tukizingatia kwamba mbu wanaoambukiza Zika wako nchini kwetu na mazingira yaliyoko nchini kwetu hayatofautiani sana na yale ya Amerika ya Kusini na nchi kama Thailand ambako ugonjwa huo unapatikana," amesema Dk. Malecela.
"Ugunduzi huu tumeupata kwa watu na tutaendelea kufanya kazi kuangalia kama tutaupata kwa mbu ambao utatuhakikishia basi kwamba ugonjwa huo ina maana umekuwepo nchini ni vile tu ulikuwa haujaonekana."
"Heri nusu shari kuliko shari kamili, kulielewa jambo na kujua kwamba lipo nchini na kujua kwamba wajawazito wanaweza kuzaa watoto wenye matatizo haya kutatuwezesha kuzuia ugonjwa huyu. Tutahakikisha nguvu zetu za kupambana na mbu wanaoeneza virusi hivi zinaongezeka."
Virusi vya Zika zimekuwa vikisababisha watoto kuzaliwa wakiwa na ubongo uliodumaa na vichwa vidogo katika mataifa ya Amerika Kusini na sana Brazil.
Mapema mwaka huu, serikali ya Tanzania iliwaagiza madaktari wote kuwa macho kuhusu hatari ya virusi hivyo mlipuko ulipotokea nchini Brazil.
Virusi vya Zika huenezwa sana na mbu ingawa kumeripotiwa pia visa vya watu kuambukizwa virusi hivyo kupitia kufanya mapenzi.
Haijabainika iwapo aina ya virusi vya Zika vilivyopatikana Tanzania ni vile ambavyo vimekuwa vikisababisha watoto kuzaliwa na vichwa vidogo Amerika Kusini.
Dalili za virusi vya Zika
Virusi vya aina hiyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza barani Afrika katika visiwa vya Cape Verde mwezi Mei mwaka huu.
Jina la virusi hivyo linatokana na msitu wa Zika, Uganda ambapo virusi hivyo vilitambuliwa kwa mara ya kwanza 1947.
Wengi wa walioambukizwa aina ya awali ya virusi walikuwa wakipatwa na homa ambayo si kali sana, mwasho na maumivu katika maungio.
Lakini kwa aina ya sasa, ambayo mlipuko wake ulianza mwishoni mwa mwaka 2015 nchini Brazil, dalili zake zimekuwa kali na virusi hivyo vinaaminika kusababisha kudumaa kwa ubongo na kasoro nyingine mwilini.
0 Michango:
Post a Comment