Na Mwandishi Wetu
BAADA ya kushinda pingamizi la kutokusoma shitaka la kwanza na tano yaliyowekwa na upande wa utetezi katika kesi ya uchochezi inayomkabili, Tundu Lissu, Jabir Idrissa, Simon Mkina na Ismail Mahaboob, upande wa Jamhuri umesomea mashitka hayo upya.
Lissu ni Mbunge Singida Mashariki, Simon Mkina Mhariri wa gazeti hilo, Jabir Idrissa Mwandishi mwandamizi wa gazeti hilo, Tundu Lissu Mbunge wa Singida Mashariki na Ismail Mahboob meneja wa kampuni ya uchapishaji ya Flint.
Awali tarehe 20 Septemba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilitoa maamuzi ya pingamizi hilo ambapo upande wa Jamhuri uliambiwa kuwa unauwezo wa kurudisha upya mashtaka hayo.
Leo Patrick Mwita wakili wa serikali mbele Thomas Simba Hakimu Mkazi Mkuu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, amesoma shitaka la kwanza na tano.
Mwita amedai kuwa Shitaka la kwanza ni la kupanga njama za kutoa chapisho la uchochezi, kosa linalodaiwa kutendwa kati ya tarehe 12 na 14 Januari mwaka huu ambapo Idrissa, Mkina na Lissu katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam walipanga njama za kuchapisha taarifa za uchochezi.
Katika kosa la tano, mshitakiwa namba moja (Idrissa), namba mbili (Mkina) na namba nne (Lissu), wanatuhumiwa kuchochea hofu miongoni mwa wananchi kwa kuchapisha habari “Machafuko yaja Zanzibar” na kwamba habari hiyo ingeweza kuzua vita au umwagaji damu.
Mashtaka hayo yalikuwa yanapingwa na mawakili wa upande wa utetezi kwa hoja ya kuwa na upungufu wa kisheria ikiwa pamoja na kutokuwa na kibali cha mwendesha mashtaka wa serikali.
Upande wa Jamhuri ulilazimika kusoma shitaka matatu ambalo ni la pili, tatu na nne.
Shitaka la pili likimkabili Jabir, Mkina na Lissu, wakidaiwa kuchapisha chapisho la uchochezi katika Gazeti la MAWIO, toleo Na. 182 la tarehe 14-20 Januari 2016.
Shitaka la tatu linamuhusu Ismail akidaiwa kuchapisha chapisho la uchochezi katika gazeti hilo lenye kichwa cha Habari "Machafuko yaja Z’bar."
Shitaka la nne linamkabili Ismail akidaiwa kuchapisha gazeti bila kupeleka kiapo kwa Msajili wa Magazeti.
Upande wa Jamhuri umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo wameiomba Mahakama ipange tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 18 Januari mwaka 2017.
0 Michango:
Post a Comment