RAUNDI ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) inatarajia kuendelea mwishoni mwa wiki hii ya Novemba 27 huku mchezo mmoja ukichezwa jana kati ya Baruti ya Mara na Ambassador ya Simiyu iliyokubali kipigo cha mabao 3-1 mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Halmashauri Kahama.
Mechi zinazotarajiwa kuchezwa mwishoni mwa wiki hii ni Tomato dhidi ya Jangwani katika mchezo utakaofanyika mkoani Njombe.
Mbuga FC ya Mtwara itacheza na Muheza United huko Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara huku Kabela City ya Kahama itakuwa mwenyeji wa Firestone ya Kiteto mkoani Manyara.
Raundi ya tatu itafanyika Desemba 3, 2016 kwa kukutanisha timu za Mtwivila ambayo itasubiri mshindi kati ya Tomato na Jangwani wakati Stand Bagamoyo itasubiri mshindi kati ya Mbuga na Muheza United ya Tanga huku Stand Misuna inasubiri mshindi wa mchezo kati ya Kabela City na Firestone ya Manyara ilihali Mrusagamba ya Kagera sasa inasubiri kucheza na Baruti ya Mara.
Kufika hapo Tomato iliing’oa Mkali ya Ruvuma kwa ushindi wa penalti 6-5; Jangwani iliifumua Nyundo 2-0; Mtwivila iliilaza Sido kwa mabao 7-4; Mbuga iliifunga Makumbusho mabao 5-4; wakati Muheza ilishinda 2-1 dhidi ya Sifa Politan ya Temeke.
Timu ya Stendi FC ililala kwa Kabela City kwa mabao 5-3; wakati Stand Misuna iliifunga Veyula mabao 2-1 huku Stand ikiilaza Zimamoto mabao 5-4 ilihali Baruti FC ya Mara na Mrusagamba ya Kagera zilipita baada ya wapinzani Gold Sports ya Mwanza na Geita Town kugomea mechi za awali kwa kutojitokeza uwanjani.
0 Michango:
Post a Comment