Kanuni muhimu ya
kulinda ajira yako ni kuishi kama mfanyakazi.
Matokeo ya ama kudumu
kazini au kupoteza kazi, hutokana na aina ya maisha ambayo unakuwa
umejichagulia.
Kila tabaka lina aina
ya maisha ambayo limejichagulia. Mathalani, kwa wanamuziki, muda mwingi wa
mchana unaweza kuwakuta wamelala, lakini usiku wanakuwa kwenye majukumu yao
yanayowaingizia kipato.
Siyo jambo la ajabu
kukutana na mwanamuziki usiku wa manane akiwa klabu. Akitoka hapo anakwenda
kulala. Mizunguko ya usiku ni aina ya maisha ya wanamuziki. Usiku ndiyo mchana
wao. Akaunti zao benki hunawiri kwa namna wanavyowajibika usiku.
Wachimbaji na
wafanyabiashara wa madini, wao majukumu yao ni ya msimu zaidi. Wakipata leo
wanaweza kuchukua muda kupata mawe mengine ili wayauze. Hao unaweza kuwakuta
wamelewa mchana na usiku. Wanaita kujipongeza kwa kazi nzuri na uvumilivu.
Yapo makundi mengi
ambayo ratiba zao za kulala na kuamka haziwabani. Hawana daftari la kusaini
mahudhurio kila asubuhi mapema wala hawasaini alama ya vidole kwa kampuni
zinazotumia mashine za kielektroniki.
Tambua ajira yako
Umeona makundi
mbalimbali na maisha yao. Jiulize unafanya kazi gani? Kama unapaswa kuamka
asubuhi kuwahi kazini kisha ukawa unashindana na wenye kukesha kumbi za
starehe, hakika kazi yako itakushinda.
Watu wengi wamekuwa
wakishindwa kutofautisha ajira zao na za wengine. Mtu anaamka asubuhi kuwahi
kazini, akitoka harudi nyumbani anaunganisha kumbi za starehe na kurejea
nyumbani alfajiri. Anafika na kubadilisha nguo kisha anaeleka kazini.
Ratiba anayojiamulia
inamfanya aishi kwa shida kazini. Anafika kazini akiwa amechoka, utendaji wake
unakuwa wa ovyo kwa sababu apati muda wa kupumzika, matokeo yake anaharibu kazi.
Mwingine kutokana na
maisha ya nje ya kazi anajikuta kila siku anachelewa kufika kazini. Tabia hiyo
inamfanya agombane na viongozi wake kila siku. Mara kwa mara anapokea onyo la
mdomo au la barua kutoka kwa meneja rasilimali watu.
Ulipotoka kazini
ulijumuika na marafiki ukalewa mpaka karibu na asubuhi. Unapoingia kazini
unakosa ufanisi. Unakuwa na mawenge mengi kutokana na mwangwi unaokuwepo
kichwani, unaosababishwa na matukio ya usiku kucha.
Wakati mwingine
unaingia kazini ukiwa na kiwango kilevi au kwa kuzidiwa na usingizi pamoja na
uchovu, unashindwa kuendana na wafanyakazi wenzako. Yote hayo ni mambo ya
kuzingatia.
Mtu wa aina hiyo
anapofukuzwa kazi, hawezi kusingizia kuwa kilichosababisha ni mazingira ya
kazini, bali maisha yake nje ya kazi ndiyo yanakuwa yamemtengenezea matokeo ya
kusitishwa kwa ajira yake.
Nje ya hehaheka za usiku
Unaweza ukawa si mtu
hekaheka za usiku. Hata hivyo, bado aina ya maisha yako nje ya kazi yakawa na
gharama kubwa kwenye ajira yako.
Mathalani, nje ya kazi
una marafiki ambao mnazungumza lugha chafu isiyovumilika, ukiwa kazini
unajikuta unamtamkia maneno machafu mfanyakazi mwenzako.
Nje ya kazi unakuwa na
watu wapenda umbea na utesi. Nawe unazoea tabia hizo, kwa hiyo unakuwa mwingi
wa kuteta wenzako kazini na kuchonganisha wafanyakazi wenzako mpaka tabia hiyo
inakugharimu.
Unakuwa na matumizi
makubwa nje ya kazini kwako. Kwa hiyo unajikuta unakuwa mtumwa wa madeni.
Wanaokudai wanakusumbua mpaka unashindwa kutulia kazini utimize majukumu yako.
Umeajiriwa ufanye kazi
na menejimenti inahitaji kuona matokeo ya ajira iliyokupa. Wewe unageuka
kituko, viongozi wako wanakuona mzigo. Unadhani watakuvumilia mpaka lini?
Hakitapita kipindi kirefu watakuondoa kazini.
Ukiwa nje ya ajira,
fahamu kuwa aina ya maisha uliyokuwa unaishi nje ya kazi ndiyo yamegharimu
ajira yako. Lazima utambue nafasi yako na uitumikie inavyotakiwa.
Unafanya kazi za
utendaji. Muda wote unatakiwa uwe unakimbizana na kazi. Kwa vile nje ya kazi
umezoea kupiga soga na marafiki, matokeo yake ukiwa kazini unakuwa mtu wa
maongezi kuliko kazi.
Siku utakapopokea barua
ya kusitishiwa ajira yako, hutakiwi kumtafuta mchawi, bali rejea mazingira yako
ya kupenda kusogoa nje ya kazi halafu unganisha na jinsi tabia hiyo ulivyoingia
nayo kazini.
Tengeneza mazingira bora
Ukishakuwa kwenye
ajira, hakikisha unatengeneza mazingira bora yatakayokubeba kwenye kazi yako.
Tumia muda nje ya kazi kujielimisha zaidi kuhusu kazi unayofanya pamoja na
kupumzika.
Tenga muda wako vizuri
na uhakikishe unapoingia kazini unakuwa sawasawa kimwili na kiakili. Jiweke
mbali na ratiba za kukuchosha kimwili na kiakili. Unapoingia kazini unapaswa
kweli uonekane umeingia na nguvu mpya. Si jambo la kuvutia kwa mfanyakazi
kuingia kazini asubuhi ukiwa umechoka, utafanyaje kazi?
Lazima utambue kuwa
yapo maisha ya wakeshaji wa usiku na uamue kuwa hayo si ya kwako. Itazame kazi
yao kwa nidhamu, halafu maisha yako nje ya kazi uyafanye yafanane na hiyo kazi
yako.
Usiishi kama
mwanamuziki kila usiku uwe kumbi za starehe wakati wewe ni ofisa wa benki.
Usimuige muuza dawa za kulevya kuishi kwa anasa nyingi, wakati unategemea
mshahara wa mwisho wa mwezi.
Unaweza kushawishika
uanze wizi ambao siyo tu utakuharibia kazi bali pia unaweza kujikuta uko
kifungoni. Kondakta wa daladala akiwa kazini kwake anazungumza sana, ila wewe
ni nesi unahudumia wagonjwa, kwa hiyo hutakiwi kupayuka utawaumiza wagonjwa.
Kelele unazokutana nazo nje, usiziingize kazini kwako.
0 Michango:
Post a Comment