Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, imepeleka
rasmi malalamiko yake nchini Kenya kwa kukiuka taratibu za biashara katika
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari leo
(Jumatano) na Katibu Mkuu, Biashara na Uwekezaji, Adolph Mkenda imeeleza kuwa
hatua hiyo imechukuliwa baada ya Kenya kupiga marufuku uingizwaji wa gesi ya
kupikia kutoka Tanzania na kutoza kodi unga wa ngano unaotoka nchini.
“Walizuia
gesi hiyo na kusema kuwa gesi itakayoruhusiwa kuingia Kenya ni ile itakayokuwa
imepitia Bandari ya Mombasa peke yake,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imesema kuwa baada ya kusoma taarifa
hizi Serikali ya Tanzania iliwasiliana na Serikali ya Kenya ili kupata maelezo
kuhusu hatua hii ambayo ni kinyume cha taratibu za kibiashara katika Jumuiya ya
Afrika ya Mashariki.
Pia taarifa hiyo imeeleza kuwa Mei 18 mwaka huu,
Serikali ya Kenya ilitekeleza uamuzi wake kwa kuzuia shehena ya gesi isiingie
Kenya kutokea Tanzania.
“Hatua hii
ina athari kubwa kwa wafanyabiashara wa gesi ya kupikia hapa nchini pamoja na
watu wote ambao ajira zao zinategemea biashara hii,” imesema taarifa hiyo.
Imesema suala hilo lilijadiliwa kwa kina katika
kikao cha Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na
Uwekezaji la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kilichofanyika Juni, 2017 na
kufanyiwa maamuzi.
Imesema Serikali ya Kenya ilikubali kuondoa katazo
la uingizaji wa gesi kupitia Tanzania mara moja na makubaliano haya yaliingizwa
kwenye kumbukumbu za mkutano ambazo ziliafikiwa na nchi zote wanachama wa
Jumuiya kwa kuweka sahihi.
Pia imeeleza kuwa pamoja na makubaliano hayo, Kenya
imeendelea kuzuia gesi isiingie nchini mwao kutokea Tanzania. Serikali ya
Tanzania imewasilisha
rasmi malalamiko yake Kenya kuhusu suala hili.
0 Michango:
Post a Comment