Na Mwandishi wetu
BALOZI wa Tanzania katika Muungano wa Visiwa vya Komoro, Mhe. Sylvester M. Mabumba mapema wiki hii alikabidhi hati za utambulisho kwa Rais wa Muungano wa Visiwa vya Komoro Mhe. Azali Assoumani. Hafla ya kukabidhi hati hizo ilifanyika kwenye Ukumbi wa Ikulu ya Komoro ijulikanayo kama Beit.
Wakati akihutubia, Mhe. Mabumba alijitambulisha kwa Mhe. Rais na kueleza furaha yake ya kuteuliwa kuwa Balozi wa pili kutoka Tanzania kuja kutumikia nchini Komoro. Aidha, alieleza furaha yake kwa mapokezi mazuri aliyoyapata tangu kuwasili kwake Visiwani humo na kwamba yamemfanya ajisikie yupo nyumbani.
Alieleza kuwa anatambua kazi kubwa iliyopo mbele yake na kuahidi kuwa katika kipindi chake wakati akiwa Balozi nchini humo atajitahidi kukuza mahusiano yaliyopo baina ya Tanzania na Komoro. Sambamba na hilo, Mhe. Balozi alieleza dhamira yake ya kutaka kuona mahusiano baina ya nchi hizi mbili yanakuwa na manufaa kwa pande zote halikadhalika kukua kwa uhusiano wa kindugu kwani mahusiano baina ya Tanzania na Komoro ni ya kihistoria.
Pia Mhe. Rais Assoumani katika hotuba yake naye alianza kwa kuonyesha furaha yake ya kuwasili kwa Balozi pamoja na kukiri kupokea barua ya kurejea Balozi aliyepita na ya kuwasili kwa Balozi wa sasa. Vilevile alieleza kuwa kila Mkomoro hujisikia nyumbani pindi anapo tembelea Tanzania kutokana na ukarimu wanao onyeshwa wanapokuwa huko. Aidha Mhe. Rais alimuhakikishia Mhe. Balozi kuwa atarajie kupata ushirikiano wake pamoja na wa Serikali yake katika kipindi chote atakapo kuwa nchini humo.
Mhe. Balozi Mabumba alitumia fursa hiyo pia kumuomba Mhe. Rais Assoumani kufanye ziara ya kikazi nchini Tanzania ili kuweza kudumisha mahusiano yaliyopo baina ya nchi hizo mbili.
0 Michango:
Post a Comment