Maalim Seif Shariff (wakwanza) akiwa na Askofu Gwajima |
Na mwandishi wetu
MMCHUNGAJI wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima amemuweka kiporo Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba na kuhoji kwa nini mwenyekiti huyo anaruhusiwa kukivuruga chama hicho.
Askofu Gwajima ameyahoji hayo baada ya kupokea malalamiko ya mgogoro uliopo ndani ya CUF kutoka kwa Katibu Mkuu wa chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad alipokwenda kumtembelea ofisini kwake, leo Ubungo jijini Dar es Salaam.
“Katika mazungumzo yetu nilitaka kujua Lipumba anafanyaje kuvuruga chama chako ili nami nijue cha kufanya, si unajua tena. Kwa nini unamruhusu kukivuruga chama?” amehoji Gwajima.
Baada ya kuhoji hayo, Gwajima amesema atayatafakari mazungumzo hayo na kwamba baada ya kutafakari atajua cha kufanya sambamba na kuueleza umma kile atakacho kuwa nacho.
“Kwa vile ameniambia mgogoro jinsi ulivyo basi nami najua cha kufanya, na nitakacho kuwa nacho nitasema baadae, ngoja nitafakari kwanza,” amesema.
Kwa upande wake Maalim Seif ambaye alizuru kwa Gwajima kwa ajili ya kumjulia hali na kuzungumza naye masuala mbalimbali ya nchi, amesema anamuunga mkono mchungaji huyo kwa chochote atakacho kufanya.
“Namuunga mkono aliyoyasema, sisi ni marafiki wa muda mrefu nimekuja kumjulia hali na kuzungumza naye mambo mbalimbali na kila mmoja kayaeleza yake,” amesema Maalim Seif.
0 Michango:
Post a Comment